NAIBU Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel na Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, wamewatembelea wagonjwa katika Kituo Cha Afya cha Mwangika wakati wa ziara ya waziri huyo jimboni hapo.
Katika ziara hiyo, Dk. Mollel amezungumza na watumishi wa Idara ya Afya wa Halmashauri ya Buchosa na watumishi wa kituo hicho ambapo amewaeleza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na kuwa na nidhamu ya kazi huku akiwasisitiza kuwa na matumizi mazuri ya dawa na vifaa tiba vinavyoletwa na serikali kwa ajili ya wananchi.

Amesema serikali haitamuacha salama mtu yeyote ambaye anafanya kazi ya kuiba dawa au vifaa tiba kwani inaingia gharama ya mabilioni ya fedha kununua dawa hizo kwa ajili ya wananchi wake na si kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache wanaoihujumu serikali na wananchi wanyonge.

Naye Mhe. Shigongo amesema endapo Hospitali ya Wilaya iliyopo Isaka ikianza kufanya kazi, itasaidi kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Kituo cha Mwangika na kupanua wigo wa huduma hiyo, hivyo kuokoa maisha ya wananchi wengi wanyonge tofauti na ilivyo sasa.
Aidha, ameiomba Wizara ya Afya kupeleka fedha, vifaa na madawa ili Hospitali ya Wilaya ya Isaka ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Baada ya ombi hilo, Dk. Mollel ameagiza Hospitali ya Isaka, kufikia mwezi ujao wa Aprili, ianze kutoa huduma kwa wananchi.
“Tayari serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa mbalimbali kwa ajili ya hospital hii ya Isaka. Ni vyema huduma za kawaida zikaanza kutolewa kwa wananchi.

“Serikali italeta vifaa vyote muhimu ili wananchi waweze kutibiwa na kufanyiwa upasuaji hapa hapa. Malengo ya serikali ni kusogeza huduma karibu na wananchi na hii ndiyo inatupeleka katika uchumi wa kati ambao nchi yetu imefikia. Tunataka wananchi wetu wasipate shida ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya,” amesema Mollel.