
Maombi ya kuzuia mchakato wa Uchaguzi wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuendelea ikiwemo maandalizi na kampeni wakati kesi ya msingi ikiendelea yamekataliwa Katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Uamuzi huo umetolewa leo Julai 2, 2020 mbele ya Jaji wa mahakama hiyo, Edwin Kakolaki baada ya kupitia hoja za pande zote mbili zinazopingana.
Jaji Kakolaki amesema kuwa mlalamikaji aliomba zuio la muda la mchakato wa uchaguzi, katika hati yake ya kiapo alishindwa kuishawishi mahakama kukubali maombi yake, kutokana na hoja hiyo maombi ya zuio yamekataliwa, wajibu maombi watatakiwa kuwasilisha majibu ya madai ya mlalamikaji Julai 6, 2020 na mlalakaji atawasilisha majibu kama yapo Julai 8 mwaka huu na kesi itaanza kusikilizwa Julai 9, 2020.
Mlalamikaji katika shauri hilo ni Ally Salehe na mlalakiwa ni Bodi ya Wadhamini ya TFF, TFF na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi.
Wakili wa Mlalamikaji, Frank Chacha anaiomba mahakama kukubali maombi ya kusimamisha mchakato wote wa uchaguzi kwa muda wakisubiri usikilizwaji wa kesi ya msingi ya kusimamisha uchaguzi huo.