
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, leo Juni 6, 2024 amefanya mahojiano na kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia Global Radio na Global TV, na ametoa ufafanuzi kuhusu bandari na mkopo wa shilingi trilioni 6.7 (Dola bilioni 2.5) kutoka Korea.
Matinyi amesema mkopo huo nafuu umetolewa baada ya Rais Samia Suluhu Hassani kufanya ziara katika nchi hiyo na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 59 tulionufaika.
Alisema katika ziara hiyo Tanzania na Korea zimewekeana mkataba na kuandikiana hati ya makubaliano ambapo cchi hiyo ya Korea itafanya utafiti mbalimbali nchini wa madini na baharini.hivyo hakuna kitu kilichowekwa rehani.

Alisema Korea inatengeneza magari yasiyotumia mafuta na badala yake yanatumia betri na malighafi ya hizo betri yanapatikana hapa nchini, hivyo tumewataka waje wafanye utafiti kuhusu madini yetu hayo.
Alisema pia kuna mpango wa kuthaminisha madini hapahapa nchini kwa maana badala ya kupeleka madini hayo kama yalivyo, yatengenezwe bidhaa hapahapa nchini na kusafirishwa kama bidhaa.
Alisema pia kuna mkataba wa kuboresha mazao ya bahari kama samaki ambapo watatuletea meli za kisasa na kutakuwa na bandari ya uvuvi huko Bagamoyo ambako samaki wote watapelekwa kiwandani humo ambako minofu itasafirishwa baada ya kupitia kiwandani.
Alisema Tanzania na Korea zitajenga vyuo viwili Dodoma kwa ajili ya kukuza teknolojia ya kisasa kwa vijana wetu na kujifunza utafiti na kujenga viwnda.
Stori na Elvan Stambuli, Global Publishers.