×

Utendaji Kazi Kituo Cha Huduma Kwa Wateja Tanesco Wamkwaza Dkt. Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameeleza kutoridhishwa kwake na Kituo cha Huduma kwa wateja cha Shirika la Umeme nchini TANeSCO na kusema huduma duni zinasababisha malalamiko kutoka kwa wateja.

Biteko amesema hayo leo wakati wa Kikao cha Tatu cha Tathmini ya Utendaji Kazi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati katika kipindi cha Oktoba-Desemba 2024 ikiwa ni utaratibu aliouanzisha kwa lengo la wa kujipima katika kila baada ya miezi mitatu ili kuboresha utendaji wa kazi wa Wizara na Taasisi zake.

“ Umeme kukatika kuna sababu zake, na kila mmoja anajua ndani anakuwa anajua. MD na Watu wa TANESCO msitupambanishe na wananchi na msichafue sura zetu, Hivi ujasiri wa mtumishi kumfokea mwananchi anaupata wapi? amehoji Dkt. Biteko.

Amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Gisima Nyamo Hanga kuhakikisha kituo hicho kinaboreshwa.

“Pamoja na kazi zote nzuri mnazozifanya lakini eneo ambalo bado hatujafanya vizuri ni utoaji wa huduma kwa wateja, juzi nilitembelea kituo hiki nikawaambia sifurahishwi na utendaji kazi wa kituo, mimi nafahamu changamoto za kituo hiki si kwa kuota bali wananchi wananipa mrejesho pamoja na viongozi wanaonisimamia, hivi tumefanya kazi yote hii ya kuwa na umeme wa ziada, tunajenga laini za umeme, lakini mtu mmoja ambaye kazi yake ni kumsikiliza mteja na kumpa majibu sahihi anatupaint wote vibaya tunaonekana hatufai, majibu yapo lakini wataalam wanageuka kuwa wababe kwa wateja, hii hakubaliki.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ametolea mfano lalamiko la mwananchi la kupiga simu TANESCO kisha akapewa tiketi namba ya lalamiko lakini baada ya muda tiketi namba hiyo ilifutwa kwa madai kwamba lalamiko husika limeshashughulikiwa huku ikiwa sikweli, hata hivyo baada ya mteja kuuliza kwa nini lalamiko lake limefutwa aliishia kufokewa.