×

Mahakama Yaamuru Dkt Slaa Alifishwe Mahakamani

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru kutolewa kwa amri ya Mwanasiasa Mkongwe, Dkt. Wibroad Slaa (76) kufikishwa mahakamani ifikapo Machi 4, mwaka huu ili uweze kutolewa uamuzi wa kesi hiyo itakuwa inasikilizwa kwa njia gani.
Uamuzi huo ulitolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema alidai kuwa shauri hilo lilipelekwa kwa ajili ya kutajwa na kueleza kuwa kwa kuwa shauri hilo lipo katika taratibu nyingine za kirufaa zinaendelea katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, hivyo aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya shauri hilo kutajwa.
Rufaa katika kesi hiyo ilikatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka juu ya uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam wa kuamuru shauri namba 993/2025 kurudishwa mahakamani hapo ili liweze kutolewa uamuzi juu ya dhamana ya Dkt. Slaa ambayo hapo awali iliwekewa pingamizi na upande wa mashitaka.
Baada ya Mrema kueleza hayo upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Melkion Sanga ulidai kuwa katika kikao kilichopita ilitolewa amri ili mshitakiwa aweze kufikishwa mahakamani siku ya leo na kujua mwenendo wa kesi yake inavyoendelea.
Sanga alidai kuwa kwa kuwa mshitakiwa hakufikishwa mahakamani aliiomba mahakama itoe ahirisho fupi ili aweze kufikishwa mahakamani kama ilivyoamuriwa katika kikao kilichopita, pia alidai kuwa amri ya mahakama ilivyotolewa ilitakiwa ifuatwe kwa mshitakiwa kufikishwa mahakamani hapo.
Akijibu hoja hiyo Mrema alidai kuwa kwa upande wa mashitaka hawakupokea amri ya mshitakiwa kufikishwa kutoka mahakamani ndiyo sababu walishindwa kumfikisha mshitakiwa mahakamani hapo.
Mrema alidai kuwa kwa mshitakiwa kufikishwa mahakamani hakuthibitishi afya yake ipo vipi kama alivyodai wakili wake, hivyo alidai kuwa mahakama inaweza kutoa uamuzi kwa kutoa amri mshitakiwa afikishwe mahakamani au kesi isikilizwe kwa mkutano wa njia ya video.