
February 11, 2025 Katika Mkutano wa juhudi za kuimarisha utoaji wa huduma za umma kwa njia za kidijitali, mkutano wa tano wa Serikali Mtandao Umeanza jijini Arusha, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Mkutano huu umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wataalamu wa TEHAMA na wadau wa maendeleo. Mgeni rasmi katika mkutano huu ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pia amegusia Mipango na maandalizi ya Siku ya wanawake Dunia ambayo inafanyika Kitaifa Mkoani humo,
“Sherehe ya Siku ya Wanawake Kitaifa Arusha tunafanya kitu cha tofauti. Kutakuwa na michezo kama mpira wa miguu, ukiwahusisha wachezaji wa kike kutoka timu za Simba Queens, Yanga Queens, JKT Queens na Fountain Gate FC. Hii ni sehemu ya juhudi za kukuza vipaji vya wanawake katika sekta ya michezo na kuwawezesha kwa njia mbalimbali.”
Maadhimisho haya yanatarajiwa kuwavutia washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, huku yakiwa na lengo la kuhamasisha usawa wa kijinsia na kuwatambua wanawake kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Mkutano wa Serikali Mtandao unaendelea, ambapo mada mbalimbali zitajadiliwa, ikiwemo ubunifu katika utoaji wa huduma za umma kupitia mifumo ya kidijitali.