
Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni amesema Umoja wa Ulaya (EU) haupaswi kuchukua msimamo ambao utakinzana na sera ya Marekani kuhusu Ukraine.
Shirika la Habari la Italia (ANSA), likiripoti juu ya mkutano wa dharura wa viongozi wa Ulaya kuhusu Ukraine uliofanyika mjini Paris wiki hii ambao Meloni alihudhuria, limesema, waziri mkuu huyo wa Italia hakufurahishwa na mfumo wa kuhusisha nchi maalumu zilizoalikwa.
Amesema ni kwa sababu haukujumuisha nchi za maeneo ya Baltic na Nordic, ambayo ndiyo yanayokabiliwa zaidi na hatari ya kupanuka kwa vita nchini Ukraine.
Meloni amenukuliwa akisema kuwa, mkutano huo hauwezi kufanywa kuwa wa “kumpinga Trump”, na akaongeza kuwa Marekani inachukua hatua ili kufikiwa amani na EU nayo inapaswa itoe mchango wake katika muktadha huo.
Wakati wa mkutano huo, Meloni alieleza msimamo wake wa kupinga matamshi ya waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer kuhusu uwezekano wa kutumwa askari wa kulinda amani wa Ulaya nchini Ukraine na akaongeza kuwa, hilo litakuwa suluhisho tata zaidi na lenye ufanisi duni.