
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC), Wafula Chebukati, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.
Kaka yake, Daniel Chebukati, amethibitisha kifo chake, akisema kuwa alifariki akiwa na umri wa miaka 63. Wafula Chebukati alikuwa amelazwa hospitalini kwa matibabu kwa zaidi ya wiki moja, ingawa sababu halisi ya kifo chake bado haijajulikana.
Chebukati alihudumu kama Mwenyekiti wa IEBC kwa kipindi cha miaka sita, kuanzia Januari 2017 hadi Januari 2023. Katika kipindi chake cha utumishi, alisimamia chaguzi tatu muhimu za kitaifa: Uchaguzi Mkuu wa 2017, Uchaguzi wa Marudio wa Rais wa 2017, na Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Rais wa Kenya, William Ruto, kupitia mtandao wa X, ameonyesha masikitiko yake, akisema kwamba ni taarifa ya kuhuzunisha. Taifa la Kenya linapoteza kiongozi muhimu ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa uchaguzi nchini.