×

Gambo Amfyatukia Makonda Kisa Ubunge wa Arusha Mjini- Video

Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo.

Kikao maalumu cha Baraza la Madiwani cha Jiji la Arusha kilichofanyika Februari 24, 2025, kimeacha gumzo baada ya baadhi ya madiwani kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kuchukua fomu ya kugombea ubunge wa Arusha Mjini.

Hata hivyo, mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Mrisho Gambo, amewajibu vikali akibainisha kuwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo ndizo zinazozua msukosuko huo.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Gambo amesema kuwa, amekuwa mstari wa mbele kulinda maslahi ya wananchi, akitoa mfano wa uamuzi wake wa kusimamia ununuzi wa ekari 6 za ardhi kwa Shilingi milioni 300 badala ya milioni 512, akihusisha taasisi za serikali kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuzuia ufisadi.

Gambo amesema hatua hiyo imewaumiza baadhi ya watu waliokuwa na mpango wa kujinufaisha, na sasa wanatafuta namna ya kumchafua kisiasa.

“Kama kuna mtu anataka ubunge, asubiri utaratibu ufike, ajitokeze uwanjani. Wananchi wa Arusha Mjini wanajua nani anawatumikia. Kuna watu wanatumia kivuli cha mamlaka zao kujaribu kunivuruga, lakini hatuna wasiwasi kwakuwa ni mzoefu kwenye siasa,” alisema Gambo.

Katika kikao hicho cha Februari 24, 2025 , madiwani wakiongozwa na Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Abraham Mollel, na Diwani wa Kata ya Themi, Petro Lobora, walimuomba Makonda kuchukua fomu ya ubunge wakidai wana imani naye. Hata hivyo, Makonda hakutoa majibu yoyote kuhusu pendekezo hilo.