
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Tundu Lissu amewaomba watanzania kukiunga mkono chama hicho kwa kukichangia kupitia mkakati wa kuchanga kidogo kidogo wa Tone Tone.
Lissu ametoa wito huo Februari 27, 2025 wakati akizindua mkakati huo na kueleza kuwa michango midogo midogo ikiunganishwa itasaidia chama hicho kupata fedha za kukiwezesha kutekeleza majukumu yake na kuwafikia watanzania wengi.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, John Mnyika ametoa wito pia kwa watanzania na wasio watanzania kuweza kujiunga na mkakati wa Tone Tone wa kukichangia chama hicho kwani wakijiunga watakuwa wamejiunga na kuchangia mabadiliko.

Mnyika akizungumza katika uzinduzi wa mkakati huo amesema michango hiyo itatumika katika kazi mbalimbali za kichama ikiwemo kuwawezesha viongozi wa chama hicho kusafiri maeneo mbalimbali nchini kuweza kuwaelimisha watanzania kuhusu sera zake na kufanay mikutano ya hadhara.
Mwenyekiti wa Kamati ndogo ye fedha wa chama hicho ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho Godbless Lema amesema wapo tayari kutumia mfumo wa sarafu za kidijitali (cryptocurrency) ili kuweza kukusanya michango ya kwenye mkakati wa Tone Tone.


