
Yapo baadhi ya matukio yanayouma mno moyo na kuacha majeraha yasiyopona.
Vuta picha kijana wako yupo nje na wenzake, wewe unaendelea na shughuli zako, lakini ghafla, unaletewa taarifa kwamba mwanao yupo mahututi kutokana na kipigo alichopata wakati akijaribu kutoa msaada!
Hii ni simulizi ya kuhuzunisha ya mama Maimuna Musa, mkazi wa Pugu Kajiungeni jijini Dar es Salaam, ambaye kijana wake, Tariq Nyumba, ameuawa kwa kipigo wakati akimsaidia mmoja wa wakazi wa mtaani kwao kufungua geti kwa ndani.
Inaelezwa kuwa Tariq aliombwa kusaidia kuruka ukuta na kufungua geti kwa ndani kutokana na jirani yao mgeni kushindwa kuingia.
Aliporuka ukuta na kuingia ndani kama alivyoelekezwa, alishambuliwa vibaya na mume wa mpangaji huyo kichwani na baadaye akapoteza maisha.
Tariq alishambuliwa Machi 21, 2025, na ilipofika Machi 23, alifariki dunia.