×

Mrisho Gambo Aibua Tuhuma Nzito Bungeni, Spika Tulia Aaingilia Kati – Video

Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, ameeleza kuwepo kwa dalili za ubadhirifu wa fedha katika ujenzi wa jengo la utawala mkoani humo, akidai kuwa vipimo vya mradi havilingani na vile vilivyoainishwa kwenye makadirio ya matumizi ya vifaa (BOQ).

Akizungumza leo Jumatano, Aprili 16, 2025, wakati wa kuchangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka wa fedha 2025/26, Gambo amesema kuna tofauti kubwa kati ya taarifa za manunuzi na utekelezaji halisi wa mradi.

Kauli hiyo ya Gambo imemfanya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson, kuingilia kati na kumtaka Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa, kufuatilia kwa kina madai hayo, ambayo aliyataja kuwa ni ya uzito mkubwa, na kutoa ripoti fupi juu ya suala hilo.

Akijibu baada ya hoja hiyo na maagizo ya Spika, Waziri Mchengerwa alisema:
“Tumezipokea hoja hizo na tutajumuisha taarifa kamili wakati wa kuhitimisha hoja. Ni muhimu kukumbushana kwamba miradi ya maendeleo haipangwi na Tamisemi pekee, bali hupitishwa kupitia vikao maalumu vya mabaraza ya madiwani, ambapo sisi wote ni sehemu ya wajumbe.”