The House of Social Media
gunners X

Maonesho ya  Kitaifa ya Kazi za Utamaduni na Sanaa Mwaka 2025 Yalivyofunguliwa

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo,  Methusela Ntonda akisoma risala kwenye ufunguzi huo. 
Ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Kazi za Utamaduni na Sanaa ya mwaka 2025 umefanyika leo, Aprili, 25,2025 jijini Dar-es-Salaam ikiwa ni maonesho ya kwanza kufanyika na kuhudhuriwa na watu zaidi ya mia Moja hamsini kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na nchi jirani kama Burundi.
Baadhi ya wadau katika ufunguzi huo.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Awamu ya sita  inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mgeni rasmi ambaye ni  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo,  Methusela Ntonda, Amesema kuwa anapenda kutoa pongezi za dhati kwa uongozi wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa maandalizi haya bora na ya mfano.
Mmoja wa Wajasiriamali anayeuza viatu aliyejitambulisha kwa jina la Rukia Chesco (kushoto), akiwaelekeza ubora wa viatu hivyo wateja waliotembelea banda lake wakati wa Maonyesho ya Kitaifa ya Kazi za Utamaduni na Sanaa yanayofanyika kwenye viwaja vya Mnazi Mmoja  jijini Dar. 
Amesema Sekta ya Utamaduni na Sanaa imeonesha ongezeko kubwa la mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hasa katika kipindi hiki ambapo dunia imeingia katika kasi kubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.
 “Sekta hii sasa imekuwa chachu ya ajira, kipato na pia ni jukwaa la kukuza utambulisho wa Taifa letu kimataifa, katika kipindi cha miaka miwili Desemba 2022 – Desemba 2024, mafanikio ya Mfuko yamejidhihirisha kupitia utoaji wa mikopo yenye thamani ya bilioni TSh 5.28 kwa miradi 359 katika mikoa 18 Tanzania Bara, utoaji wa mafunzo kwa wasanii 11,083, wakiwemo wanawake 6,739 (61%) na wanaume 4,344 (39%).
Wasanii wa Kundi la Hisia Thieta, wakionyesha uwezo wao katika maonesho hayo.
Kuchochea urasimishaji wa kazi za sanaa kwa wasanii 8,154, kupitia usajili wa biashara, namba ya mlipa kodi, kufungua akaunti za benki, kuwa na leseni na majina ya biashara nk; na Kuzalisha jumla ya ajira 449,343 zilizowanufaisha wananchi kwa zaidi ya 1,356,876.
“Na kwa mwaka huu 2025, mfuko umeandaa matukio matatu makubwa ikiwemo warsha ya wadau wa Utamaduni na Sanaa iliyofanyika tarehe 17 Aprili, 2025 katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa
iliyowakutanisha wadau 410 katika sekta ya utamaduni na sanaa.
Maonesho haya ya kwanza ya kitaifa ya kazi za Utamaduni na Sanaa ambayo leo ninayafungua rasmi, mkutano wa pili wa wadau wa sekta, unaotarajiwa kufanyika tarehe 14 Mei, 2025 na lengo la matukio haya si tu kuonesha kazi za sanaa, bali ni kujenga muingiliano thabiti utakaowezesha kazi za utamaduni na sanaa kujiendesha kibiashara, kuongeza ujumuishaji wa huduma za kifedha na matumizi ya teknolojia za kisasa kutatua changamoto za kila siku”.
Aidha amesema maonesho hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini na yameshirikisha washiriki zaidi ya 150 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na nchi jirani kama Burundi, huku zaidi ya wananchi 2,500 wakitegemewa kuhudhuria.
Huu ni ushahidi kuwa sekta hii sasa inatambuliwa kama sekta mtambuka yenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.
Matokeo tunayoyategemea kutokana na maonesho haya ni pamoja na kuongezeka kwa masoko ya bidhaa na huduma za sanaa ndani na nje ya nchi, kuimarika kwa pato la wasanii na kaya zao, kupatikana kwa mbinu mpya za uzalishaji na biashara, kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za kisasa, urasimishaji wa kazi za sanaa, kubainika kwa fursa mpya za kiuchumi kwa vijana na wanawake na kuboreshwa kwa bidhaa na huduma baada ya mrejesho kutoka kwa watumiaji.
“Kwa moyo wa dhati, nawapongeza wasanii, wajasiriamali, taasisi na wadau wote walioshiriki katika maonesho haya ambao ni Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania, Shirikisho la Filamu Tanzania, Shirikisho la Sanaa za Maonesho, Shirikisho la Muziki” alimaliza kusema,” Ntonda.

Comments are closed.