×

Suluhisho Katika Sekta ya Usafirishaji Nchini Sasa Lapatikana

Meneja Masoko na mauzo wa kampuni ya TATA ,Smart Deus (katikati)akizungumza wakati wa uzinduzi wa Trela za mizigo aina ya TIVA maalumu kwa ajili ya mizigo mikubwa jijini Dar es salaam.
Kampuni ya magari ya TATA Tanzania imezindua mpango  maalum  kwa ajili ya sekta ya usafirishaji  wa mizigo mikubwa  nchini kwa kuzindua Trela za mizigo aina ya ‘Tiva Trela’ ili kumrahisishia  mfanyabiashara na mkulima  katika kupakia mizigo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi  uliofanyika kwenye  ofisi za kampuni hiyo, Vingunguti jijini Dar es Salaam,  Meneja Mauzo na  Masoko, Smart Deus amesema  lengo  la mpango huo ni kuwaweka karibu wateja na kampuni katika  msimu  huu wa mauzo  na mavuno nchini ambapo magari hayo yanapatikana kwa mkopo pia.
Meneja Masoko na mauzo wa kampuni ya TATA ,Smart Deus (kulia)akizungumza wakati wa uzinduzi wa Trela za mizigo aina ya TIVA maalumu kwa ajili ya m,izigo mikubwa jijini Dar es salaam.
“Uzinduzi huu umeambatana  na utambulisho wa Trela ya kubebea mizigo mikubwa kwa wakati mmoja. Pia tumeandaa mpango maalum  kwa wateja watakaowahi kipindi hiki cha mwanzo kuna mikopo isiyo na riba na ile ambayo dhamana  ni kifaa husika kwa kushirikiana na taasisi za fedha  kuelekea msimu wa Mauzo na mavuno nchini kuelekea msimu wa mauzo,” amesema.
Ameeleza kuwa kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia  Suluhu Hassan, umekuwa ni wakati mzuri kibiashara kutokana na milango ya kibiashara kufunguka.
Deus amesema kutokana na hali hiyo wameahidi kushirikiana na Serikali na wadau wao kwa kuleta bidhaa bora zaidi zinazokidhi mahitaji ya Watanzania.
Amesema kwa zaidi ya miaka 20 ya kampuni hiyo nchini, wamebaini uwepo wa changamoto katika usafirishaji kulingana na mazingira na barabara, hivyo kuja na suluhisho la kuleta magari yenye uwezo wa kuendana na mazingira hayo.
Naye  Meneja Mauzo wa TATA, Kitengo cha Force Motors, Robert Mwakabibi amesema mapinduzi hayo hayajaacha nyuma usafirishaji wa abiria baada ya kuleta gari salama kupunguza adha ya usafiri na kuwaongezea kipato wamiliki na madereva wa daladala.
 Kwa upande wa magari ya shule amesema  wamebaini magari mengi hayakutengenezwa na mfumo mzuri kwa ajili ya wanafunzi hali iliyowapa msukumo wa kufanya mapinduzi katika sekta hiyo.
“Ukiangalia gari zetu ni tofauti na nyingine, gari nyingi zinaletwa zikiwa zina muda mrefu lakini za kwetu ni kipindi hiki hiki zinapoingia.
Gari za shule nyingi zilizopo hazijatengezwa maalum kwa ajili ya wanafunzi lakini za kwetu zina mfumo wa kuhudumia wanafunzi wa aina zote, wa kawaida na wenye mahitaji maaalum.
Kwa kuzingatia changamoto ya usafiri wa abiria, kampuni imeleta  gari bora zinazoweza kupunguza adha ya usafiri pamoja na kuongeza kipato cha wamiliki wa daladala.
“Tumeona soko linauhitaji mkubwa kwa usafiri wa wanafunzi, taasisi za serikali na binafsi,” ameeleza Mwakibibi.
Amesema wameweka mfumo mzuri wa  mteja kupata gari hizo ambapo kuna kulipa fedha taslimu na mkopo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha.
Akizungumzia jinsi mkopo wa magari hayo unavyotolewa, Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Begumisa Egbert, amesema mkopo usio na riba unatakiwa kulipa   asilimia 50 na nyingine iliyobaki  inalipwa kwa kipindi cha miezi 12.
Ameeleza kuwa mkopo mwingine ambao utakuwa na riba kidogo, unatakiwa kulipa asilimia 20 ya bei ya gari unayotaka, kisha iliyobaki inalipwa kwa kuanzia miezi sita miaka mitatu.