Wakazi wawili kutoka Kata za Kitobo na Minziro wilayani Missenyi mkoani Kagera, wamepata tumaini jipya baada ya mdau wa maendeleo, Evance Kamenge kujitolea kujenga nyumba za kisasa kwa ajili yao, ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa jamii.
Kamenge, ambaye ni mchumi na mkulima kutoka Kagera, amesema uamuzi wake umetokana na kushuhudia hali ngumu ya maisha ya watu hao ambao ni miongoni mwa wenye mahitaji maalum. Alieleza kuwa ameguswa na mazingira wanayoishi na kuamua kuwasaidia kwa vitendo.
“Niliona namna wanavyoishi kwa tabu, nikaguswa. Nikaona ni vema kutumia rasilimali nilizonazo kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha yao,”alisema Kamenge.
Ujenzi wa nyumba hizo mbili, ambazo kila moja ina vyumba vitatu, upo katika hatua za mwisho. Kamenge alieleza kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni 2025, nyumba hizo zitakuwa tayari kwa kukabidhiwa kwa wahusika.
Kamenge amesema amefanikisha ujenzi huo kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato na kwa msaada wa marafiki wake wa karibu waliomuunga mkono katika wazo hilo. Amewahimiza Watanzania wengine kuiga mfano huo wa kutoa bila kutegemea kuwa viongozi au wanasiasa.
Kwa upande wake, mmoja wa wanufaika, Bw. Biteganya Mbili kutoka Minziro, alimshukuru Kamenge kwa moyo wake wa upendo na kusema atamuombea kwa Mungu amzidishie baraka. Alisema nyumba hiyo itabadilisha maisha yake kwa kiwango kikubwa na kumpunguzia changamoto nyingi.
Evance Kamenge ni mzaliwa wa kata ya Kanyigo wilayani Missenyi, lakini amekuwa mstari wa mbele kutoa msaada hata nje ya eneo lake la asili, akiwahudumia wananchi wote kwa usawa.