×

Kamenge: Prof. Janabi Awe Chachu ya Kupambana na Magonjwa ya Milipuko Kagera

Kufuatia kuchaguliwa kwa Prof. Mohammed Janabi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Kanda ya Afrika, watu na wadau mbalimbali wa maendeleo, hususani katika sekta ya afya, wamekuwa wakitoa maoni mbalimbali juu ya uteuzi wake.

Mdau wa maendeleo kutoka Wilaya ya Missenyi na Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Evance Kamenge, alieleza matumaini yake kwamba uteuzi wa Prof. Janabi utaleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya, hasa katika maeneo ambayo yamekuwa yakiathiriwa mara kwa mara na magonjwa ya milipuko, hususan Mkoa wa Kagera.

Alisema kuwa mkoa huo unahitaji msaada wa kitaalamu na rasilimali za kukabiliana na changamoto hizo, ikizingatiwa unapakana na nchi jirani.

“Kagera imekumbwa na milipuko ya magonjwa mbalimbali kama Marburg. Tunatarajia Prof. Janabi atakuwa chachu ya kuleta wataalamu watakaosaidia kukabiliana na hali hiyo. Kagera inapakana na nchi nyingi, hususan Wilaya ya Missenyi, hivyo kuna haja ya kujenga vituo vikubwa vya afya ili kukabiliana na magonjwa ya milipuko,” alisema Kamenge.

Aidha, aliongeza kuwa uteuzi wa Prof. Janabi unatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya WHO na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mifumo ya afya, hasa katika maeneo yenye changamoto kama Kagera. Kwa uzoefu wake mkubwa katika sekta ya afya, Prof. Janabi anaweza kusaidia kuleta mabadiliko ya kweli na kuhakikisha kuwa mikoa kama Kagera ina uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko kwa ufanisi zaidi.

Ikumbukwe kuwa Prof. Mohammed Janabi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika masuala ya afya na tiba.