
Uongozi wa Yanga umesikitishwa na unalaani vikali vitendo vya kupigwa, kuchaniwa jezi na kufukuzwa uwanjani kwa mashabiki wake katika mchezo wa Fainali wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa Tarehe 25/5/2025 katika uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Yanga tunaamini kwenye uungwana katika mchezo wa soka, hivyo vitendo walivyofanyiwa mashabiki wetu vinapaswa kulaaniwa na Wadau wote wa soka nchini huku tukiziomba Mamlaka husika kuchukua hatua kali kwa wote waliohusika kufanya uhuni huo.
Vile vile, Uongozi wa Yanga unatoa pole kwa mashabiki wote waliokumbwa na kadhia hiyo na unawataka mashabiki wote wa Klabu hii, kuendeleza uungwana na kupinga chuki na uhasama unaotaka kujengwa na makusudi baina ya mashabiki hapa nchini.
Mwisho, Uongozi unawaomba mashabiki wote wa Yanga kutolipiza kisasi kwa namna yoyote ile na badala yake waendelee kuwakaribisha mashabiki wa timu nyingine kwenye mechi zetu ili tuendelee kufurahia mchezo wa soka huku tukidumisha ustaarabu wetu wa kulinda amani na usalama wa watu wote wanapokuwa uwanjani.
