
Arusha:
Stanbic Bank Tanzania imeanza rasmi ushiriki wake katika #CSOWeek2025, ikiadhimisha mwaka wa nne mfululizo wa kushiriki kwenye mjadala wa maendeleo jumuishi na endelevu. Ushiriki huu unaonesha dhamira ya benki hiyo katika kushirikiana na AZAKI kwa ajili ya maendeleo ya watu na jamii.

Doreen Dominic, Mkuu wa Kitengo cha Sekta ya Umma na Taasisi Binafsi wa Stanbic Bank, amesema kuwa benki hiyo ipo tayari kutoa suluhisho mahsusi, kujenga uwezo, na kushirikiana na AZAKI kuunda programu zenye matokeo halisi.

Katika juma hili, Stanbic Bank pia imeandaa kitivo maalum cha elimu ya fedha katika banda lao, ambapo wataalam waliothibitishwa na Benki Kuu ya Tanzania wanatoa elimu ya fedha kwa washiriki wa wiki ya AZAKI.

Aidha, Jumatano hii, benki hiyo itaendesha semina maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi na wajasiriamali wilayani Karatu, kupitia kiatamizi chake cha Stanbic Biashara Incubator.