
Uongozi wa msanii maarufu wa Bongo Fleva na burudani, Gigy Money, leo Juni 19, 2025 umetolea ufafanuzi hali ya afya ya msanii huyo, huku ukikanusha taarifa potofu zinazosambaa mitandaoni.
Katika taarifa hiyo, uongozi umeeleza:
“Ni kweli kwamba msanii Gigy Money anaumwa na anahitaji sana maombi yenu. Tunasihi wale wanaompigia simu au kwenda kwenye vituo mbalimbali vya afya kutambua kuwa kwa sasa yupo katika uangalizi wa madaktari waliobobea na anaendelea kupambana na hali yake akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.”
Taarifa hiyo pia imekanusha uvumi kuwa Gigy Money amepigwa au kuhusika katika ugomvi wowote, na kuwataka wananchi na mashabiki kupuuza taarifa hizo zisizo za kweli.
“Habari za kuhusishwa na mapigano au kupigwa ni uongo mtupu. Huu ni wakati wa kutoa faraja, kumuombea na kumuweka katika mawazo ya matumaini. Ni mama wa mtoto mmoja, Mayra, ambaye pia anamhitaji kwa afya njema.”
Uongozi wa Gigy Money umetoa shukrani kwa madaktari wote, taasisi za afya na watu wote waliotoa msaada na kuonyesha upendo katika kipindi hiki kigumu.
Kwa sasa, msanii huyo yupo kwenye mapambano ya kiafya, akihitaji mapumziko, amani, na maombi kutoka kwa mashabiki wake na Watanzania kwa ujumla.
