×

Orodha Fupi ya Tuzo ya SAFAL ya Kiswahili 2024 Yatangazwa Dar

Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika imetangaza orodha fupi ya miswada ya mashindano ya mwaka 2024. Tuzo hii inafadhiliwa na kampuni ya Safal Group, kupitia ALAF-Tanzania na Mabati Rolling Mills-Kenya.

Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa na Dkt. Lizzy Attree na Dkt. Mukoma Wa Ngugi mwaka 2014 ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha hizo, baina ya lugha hizo na kwa lugha hizo.

Mwenyekiti wa majaji wa mashindano ya mwaka 2024, Dkt Salma Hamad, wa Chuo Kikuu Huria, Tanzania, alisema “Miswada ilikuwa mingi hata hivyo tumeburudika vya kutosha kwa sababu tumesoma kazi zilizoandikwa na kusukwa kiubunifu na tumejifunza kwamba kuna hazina kubwa ya vipaji vya uandishi wa fasihi ya kiswahili. Vikiendelezwa fasihi ya Kiswahili haitafilisika.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo hii, Abdilatif Abdalla, aliongeza, “Ni jambo la kufurahisha mno kuona kwamba tangu mashindano yalipoanzishwa mwaka  2015, bado Tuzo hii  inaendelea kuwavutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na kwa idadi kubwa. Pia kiwango cha ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka, na kwa hivyo kuitajirisha Fasihi ya Kiswahili.”

Majaji wengine walioshirikiana na Dkt Salma Hamad kuisoma na kuwateua washindi wa mashindano ya mwaka 2024 walikuwa ni Prof. Richard Wafula wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Kenya, na Dkt. Caesar Jjingo wa Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. Jumla ya miswada iliyosomwa na Jopo la Majaji ilikuwa ni 210.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi aliyatangaza majina ya waandishi na miswada iliyoingia katika Orodha Fupi ikiwa ni pamoja na,

RIWAYA

Nderemo za Mtaa – Joel Hamisi (Tanzania)

Kitanzi cha Mauti – Mayassa Abdallah Chembea (Tanzania)

Nyaraka za Wafu – Ali Othman Masoud (Tanzania).

USHAIRI

Waadhi – Mohamed Hamid Haji (Tanzania)

Bure Ghali – Bashiru Abdallah (Tanzania)

Laana ya Uovu – Mohamed Idrisa (Tanzania)

Majaji pia waliteua mkusanyo wa hadithi fupi,

Mungu Hadanganywi na Hadithi Nyingine – Edwin Omindo (Kenya).

Alisema washindi watakaotokana na orodha hii fupi watatangazwa katika sherehe itakayofanyika tarehe 3 Julai, 2025, jijini Dar es Salaam. Zawadi za jumla ya dola za Marekani 15,000 zinatolewa kwa miswada bora zaidi ambayo haijachapishwa.

Tanzu zinazoshindaniwa ni riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia na riwaya za michoro. Zawadi zitagawanywa kama ifuatavyo:

Mshindi wa Kwanza (Riwaya) – Dola 5,000

Mshindi wa Kwanza (Ushairi) – Dola 5,000

Mshindi wa Pili (katika utanzu wowote) – Dola 2,500

Kwa mujibu wa Meneja huyo mbali na zawadi hizo, miswada iliyoshinda itachapishwa vitabu na Mkuki na Nyota Publishers, Tanzania. Na miswada ya mashairi itakayoshinda itatafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.

Alisema SAFAL Group imeendelea kudhamini Tuzo hii ya tisa kupitia makampuni yake ya ALAF- Tanzania na Mabati Rolling Mills ya Kenya kutokana na kukua kwake mwaka hadi mwaka.