
Chama Cha Mapinduzi kupitia kwa Katibu Mkuu wake Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema mwaka mpya wa Kiislamu ni fursa adhimu ya kutafakari maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W) hususani ujasiri wake, uvumilivu na moyo wake wa kujitolea kwaajili ya kuleta Haki, amani na mshikamano wa Jamii.
Balozi Nchimbi amebainisha hayo katika taarifa yake kwa Vyombo vya habari leo Alhamisi Juni 26, 2025, wakati akitoa salamu za kheri na baraka kwa Waislamu wote nchini Tanzania na duniani kote wakati huu ambao wameukaribisha Mwaka mpya wa Kiislamu 1447 Muharram.
“Kwaniaba ya CCM na kwa niaba yangu binafsi, nawatakia waislamu wote mwaka mpya uliojaa mafanikio, afya njema, amani na mshikamano. Tunathamini sana mchango wa jamii ya waislamu katika kujenga taifa letu, kukuza maadili, kuimarisha uzalendo na kudumisha umoja wa Kitaifa.” Amesema Nchimbi.
Balozi Nchimbi kadhalika amebainisha kuwa CCM inasisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wananchi, katika kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi ya amani, umoja na maendeleo kwa wote.
