
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mheshimiwa Petro Magoti amewahamasisha wananchi kutumia huduma za benki kwa maendeleo yao ya kiuchumi, kukuza biashara na kuanzisha miradi mipya.
Mheshimiwa Magoti ametoa hamasa hiyo alipozindua tawi la Benki ya CRDB wilayani Kisarawe na akaitumia nafasi hiyo kuipongeza menejimenti kwa kusogeza huduma jirani na wananchi.
“Nawapongeza sana Benki ya CRDB kwa kuwafikia wananchi wa Kisarawe, sisi seriali tutawapa ushirikiano wakati wote. Ila nitumie nafasi kuwahimiza wananchi wenzangu wa wilaya hii ya Kisarawe kuzitumia fursa zilizosogezwa kwetu na Benki ya CRDB. Tuitumie benki hii kuhifadhi fedha zetu, kuomba mikopo ya kuendeleza biashara tulizonazo na tunazopanga kuzianzisha,” amesema Mheshimiwa Magoti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul amesema tawi hilo kama yalivyo mengine zaidi ya 260 nchini kote linatoa ushauri wa biashara hivyo wananchi wasisite kulitembelea ili kupewa uzoefu wa namna ya kukuza biashara zao.
“Tunawashukuru wateja wetu wanaotumia huduma za kuhifadhi fedha na nyingine lakini benki yetu inatoa ushairi wa kibiashara ikiwamo uwekezaji. Waje hapa au katika tawi letu jingine lolote ili washauriwe namna ya kukua kibiashara sambamba na namna ya kupata mitaji ya kukuza biashara zao,” amesema Paul.