×

Kesi Ya Tundu Lissu Yaahirishwa Hadi Julai 15, 2025 – Video


Kesi namba 8607/2025 ya uhaini inayomhusu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Antiphas Lissu limeahirishwa mpaka Julai 15, 2025.

Kuahirishwa kwa kesi hiyo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi KIsutu, Franco Kiswaga kumekuja baada ya Mahakama hiyo kukubali maombi ya upande wa Jamhuri ulioeleza kuwa kwa sasa bado hawajafanya uamuzi wa kumshtaki rasmi Tundu Antiphas Lissu kwa makosa ya uhaini, shauri ambalo litafunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Awali kabla ya kutolewa uamuzi huo na mahakama, Tundu Lissu wakati akijitetea aliiomba Mahakama kuagiza upande wa Jamhuri kulipeleka shauri lake Mahakama Kuu ya Tanzania haraka kama wamekamilisha ushahidi au Mwendesha Mashtaka aonyeshe nia ya kutoendelea na shauri lake, hivyo amuachie huru (nolle prosequi).

Alimumbia Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga na asikubali kuiahirisha kwa kuwa upelelezi umechukua muda mrefu na aliwaambia waendesha mashitaka kwamba kule aliko (gerezani) sio kuzuri kuishi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga alisikiliza hoja za pande zote na alikubaliana na upande wa Jamhuri huku akiagiza taarifa juu ya uamuzi umefikia wapi itoke Julai 15 kesi hiyo itakapoendelea.

Alipoulizwa na Hakimu Kiswaga kama kuna mabadiliko juu ya malalamiko yake ya awali ya jinsi anavyoishi Gereza ya Ukonga, Lissu alisema baada ya yeye kuwasiisha malalamiko yake kuwa hatendewi vyema gerezani hivi sasa anaendelea vizuri na yale aliyokuwa akilalamikia yamerekebishwa kwa kiasi kikubwa hivyo kumshukuru hakimu kwa kumpa nafasi ya kueleza kadhia iliyokuwa ikimkabili gerezani na sasa anaruhusiwa kufanya mazoezi uwanjani ndani ya gereza hilo.

STORI NA ELVAN SITAMBULI | GPL.