×

DESMI Africa Ltd Yaimarisha Uwepo Wake Kanda ya Afrika

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayojihusisha utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya kukabiliana na matukio ya uvujaji wa mafuta baharini DESMI Afrika, Bw. Leslie Peter Andrews (Katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mikakati ya ukuaji endelevu katika Kanda ya Afrika, kukuza vipaji vya ndani na uboreshaji wa huduma. Pamoja naye ni baadhi wa maofisa wa ngazi za juu wa kampuni hiyo nchini.
DESMI Africa, kampuni tanzu inayohusika na utengenezaji wa vifaa vya kukabiliana na matukio ya uvujaji wa mafuta baharini,  DESMI Ro-Clean, yenye makao yake makuu mjini Odense, Denmark, inajivunia kutangaza kuimarika kwa dhamira yake ya ukuaji endelevu, kukuza vipaji vya ndani, na kuboresha utoaji wa huduma, sambamba na mkakati mpana wa upanuzi wa kampuni hiyo barani Afrika.
Meneja Uendeshaji wa Kampuni inayojihusisha utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya kukabiliana na matukio ya uvujaji wa mafuta baharini DESMI Afrika, Bw. Philbertus Mujuni (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu madhara mbalimbali yanayosababishwa na matukio ya uvujaji wa mavuta baharini na nchi kavu na utendaji kazi wa vifaa hivyo. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa DESMI Afrika, Bw. Leslie Peter Andrews na Bw. Christopher David mmoja wa maofisa waandamizi katika kampuni hiyo.
DESMI imekuwa ikifanya kazi nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 10, na Tanzania ikiwa ni makao yake makuu Barani Afrika, hufanikisha shughuli zake katika zaidi ya nchi 20 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku kampuni tanzu nyingine ikiwa imeanzishwa hivi karibuni nchini Nigeria. Upanuzi huu wa shughuli barani Afrika unaunga mkono lengo la DESMI la kuwa karibu zaidi na wateja wake, kuhudumia mahitaji ya soko kwa haraka, na kuchangia maendeleo ya viwanda na mazingira kwa muda mrefu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayojihusisha utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya kukabiliana na matukio ya uvujaji wa mafuta baharini DESMI Afrika, Bw. Leslie Peter Andrews (wa tatu kushoto), akipiga picha ya kumbukumbu na baadhi ya maofisa wa kampuni hiyo, mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mikakati ya ukuaji endelevu katika Kanda ya Afrika, kukuza vipaji vya ndani na uboreshaji wa huduma.
Ofisi ya Tanzania imejikita kama kitovu muhimu cha shughuli za DESMI Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikihudumia sekta mbalimbali zikiwemo baharini na pwani, mafuta na gesi, waendeshaji wa mabomba na bandari, miongoni mwa zingine. Ofisi hii ina timu ya wataalamu wa kiufundi, huduma za usaidizi wa kiteknolojia, uhakika wa upatikanaji wa vipuri, pamoja na huduma ya moja kwa moja kwa wateja, hali inayopunguza muda wa kusimama kwa mashine na kuboresha utendaji kazi.
Moja ya nguzo kuu ya mkakati wa DESMI Africa ni uwekezaji wa kina katika maendeleo ya wafanyakazi wa ndani. Kupitia ofisi ya Tanzania, DESMI imeanzisha programu za mafunzo ya ndani zinazolenga kuwawezesha wahandisi, mafundi na timu za huduma kupata ujuzi wa hali ya juu. Mafunzo haya yameundwa si tu kwa ajili ya kuhakikisha uelewa wa kina wa vifaa vya kisasa vya DESMI, bali pia kusaidia ajira ya muda mrefu na kuwawezesha kiufundi vijana wa Afrika.
“Tunaamini kwamba maendeleo endelevu hayawezi kutenganishwa na uhamishaji wa maarifa na mbinu za mafunzo,” alisema Leslie Peter Andrews, Mkurugenzi Mtendaji wa DESMI Africa. “Uwekezaji wetu Tanzania si miundombinu pekee, ni kuhusu watu. Tumejikita katika kuwezesha timu za ndani kutoa huduma bora za kiwango cha kimataifa na kuchangia kwa namna chanya katika maendeleo ya ukanda huu.”
Aliongeza, “Tumefanya utafiti wa kina kabla ya kuamua kuja kuwekeza hapa nchini, kuna bandari nzuri yenye miundombinu bora, kuna mfumo mzuri wa elimu unaotuwesha kufanikisha ujuzi wa kiufundi tunaohitaji, ina usalama wote tunaohitaji, miundombinu tunayohitaji, eneo zuri, nchi inafaa kuwekeza kwa kipindi kirefu kwani kuna utulivu wa kisiasa, na ndio maana tupo kwa miaka 10 sasa.”
Ukuaji wa DESMI barani Afrika unachochewa na ongezeko la mahitaji ya mifumo imara, yenye ufanisi wa nishati, kwa ajili ya kulinda mazingira. Kuanzia udhibiti wa mafuriko, matibabu ya majitaka, kukabiliana na uvujaji wa mafuta baharini, hadi usafirishaji wa vimiminika viwandani, suluhisho za DESMI zinasaidia miundombinu muhimu na juhudi  uendelevu kote barani Afrika.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari ofisini kwao, jijini Dar es Salaam kuhusu madhara ya uvujaji wa mafuta baharini na nchi kavu, Meneja Uendeshaji wa DESMI Afrika, Bwana Philbertus Mujuni alisema, “Inapotokea mafuta yamemwagika baharini, kwenye mito ama maziwa, athari zake ni kubwa sana,kuna Wanyama na mimea vinavyoishi baharini na nchi kavu, inapotokea mafuta yamwemwagika, mimea na viumbe hai vitakufa ama kuondoka katika mazingira hayo hivyo kuathiri pia uoto wa asili wa eneo husika na kutopatikana tena.
“Ili kuzuia hayo yasitokee ni lazima kuwe na vifaa,  ndio maana sisi kama DESMI tumekuja na teknolojia inayoweza kusaidia kuzuia hili tatizo la kumwagika mafuta, kusambaa na kuathiri mazingira lisiweze kutokea.”
Uwepo wa kampuni hii moja kwa moja nchini Tanzania pia utawezesha ushirikiano na serikali za mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali, na sekta binafsi katika miradi inayohusu mazingira na maji, hatua inayoenda sambamba na kaulimbiu ya kampuni: “Suluhisho safi kwa dunia bora.”