
Dar es Salaam, 3 Julai 2025 – Stanbic Bank Tanzania leo imewazawadia wateja 28 waliobahatika zawadi mbalimbali za fedha taslimu hadi kufikia TZS 500,000 kupitia droo ya pili ya kampeni yake ya Salary Switch. Droo hii imefanyika ikiwa ni miezi miwili tangu kuzinduliwa rasmi kwa kampeni hiyo ambayo inalenga kuhamasisha wafanyakazi nchini kuhamishia mishahara yao kwenye akaunti za Stanbic Bank.
Tukio hilo limefanyika katika makao makuu ya benki jijini Dar es Salaam na limeshuhudiwa rasmi na Bi. Irene Kawili, mwakilishi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, pamoja na wanahabari—ikiwa ni uthibitisho wa dhamira ya benki ya kudumisha uwazi na uadilifu katika mchakato mzima.
Akizungumza katika hafla hiyo, Sarah Odunga, Meneja wa Thamani kwa wateja Benkiya Stanbic, alisema “Tunaendelea kuhamasika na mwitikio mkubwa na imani ambayo wateja wetu kote nchini wanaendelea kutuonesha. Droo hii ni sehemu ya ahadi yetu ya kuwapatia thamani ya kweli wale wanaochagua kuhamishia mishahara yao Stanbic. Kwa kufanya hivyo, wanapata si tu huduma za kifedha, bali pia fursa halisi za maendeleo.”
Kampeni ya Salary Switch inatoa manufaa mbalimbali kwa wateja wanaoshiriki, yakiwemo uwezo wa kupata mkopo wa mshahara hadi asilimia 60 ya kipato chao, bima ya msiba bure kwa ajili ya mteja na familia yake, pamoja na ushauri binafsi wa kifedha kupitia programu maalum ya Financial Fitness Academy ya benki. Aidha, wateja hushiriki moja kwa moja kwenye droo za kila mwezi zenye zawadi za pesa taslimu, hivyo kuongeza thamani halisi ya mshahara wao kila mwezi.
Washindi 28 waliotangazwa leo walichaguliwa kutoka kwa kundi la wateja waliotimiza vigezo katika mwezi uliopita, wakiwa wanawakilisha mikoa mbalimbali nchini Tanzania.
Ambikile Mutembei, Meneja Uendelezaji Biashara Wateja Binafsi, Benki ya Stanbic, aliongeza “Tukiadhimisha miaka 30 ya kuwawezesha watu binafsi na biashara hapa Tanzania, kampeni hii inaonyesha azma yetu ya kuendelea kuwa benki inayomjali mteja. Salary Switch siyo tu promosheni – ni uthibitisho wa dhamira yetu ya muda mrefu ya kutembea pamoja na mteja katika safari yake ya kifedha.”
Kampeni ya Salary Switch inaendelea katika matawi yote ya Stanbic Bank nchini, na droo zaidi pamoja na zawadi za kuvutia zinatarajiwa katika miezi ijayo.