
Dar es Salaam, Tanzania – Kiungo mshambuliaji wa Klabu ya Yanga SC, Clatous Chama, anatajwa kuwa kwenye rada za klabu ya Zesco United ya Zambia, huku mkataba wake wa mwaka mmoja na Yanga ukiwa umefikia tamati.
Chama alijiunga rasmi na Yanga SC Julai 1, 2024, akitokea Simba SC kama mchezaji huru. Wakati akiwasili, Simba SC walikuwa wamemaliza msimu katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya karibu na mchezaji huyo, mazungumzo kati ya wakala wa Chama na viongozi wa Zesco United yamefikia hatua nzuri. Kinachosubiriwa kwa sasa ni mchezaji huyo kutia saini mkataba na kutambulishwa rasmi na klabu hiyo ya Zambia, endapo Yanga SC hawatamrejesha mezani kwa mazungumzo mapya.
Inaelezwa kuwa uongozi wa Yanga SC hautajafanya mazungumzo yoyote hadi sasa na Chama, licha ya kutambua kuwa mkataba wake umeisha. Jambo hili linaashiria kwa kiasi kikubwa kwamba kiungo huyo hatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga SC katika msimu wa 2025/2026, msimu ambao klabu hiyo itashiriki michuano ya CAF Champions League – ligi inayotajwa kuwa namba nne kwa ubora barani Afrika.
Clatous Chama, ambaye aliwahi kuwa nguzo muhimu ndani ya Simba SC kabla ya kutua Yanga SC, anaendelea kuvutia klabu kadhaa barani Afrika kutokana na uzoefu wake mkubwa wa mashindano ya kimataifa.