×

Trump Atoa Onyo Kali Kwa Putin: Asema Amezidiwa na Vita ya Ukraine

Rais wa Urusi, Vladimir Putin(Kushoto); Rais wa Marekani, Donald Trump(Kulia)

Rais wa Marekani, Donald Trump, jana alitoa kauli kali dhidi ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin, akimtaja kama “mtu mkali sana,” huku akisisitiza kuwa hataki kumuita muuaji, lakini amechoshwa na ukaidi wa Putin wa kukataa kumaliza vita inayoendelea Ukraine.

Kauli hiyo ya Trump ilitolewa katika mkutano rasmi na waandishi wa habari akiwa na Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, ndani ya Ikulu ya White House, ambapo alitangaza hatua mpya na kali zaidi dhidi ya Urusi.

Katika kile kilichoonekana kama mabadiliko makubwa ya kisera kutoka msimamo wake wa awali wa tahadhari kwa Urusi, Trump sasa ameanza kuiwekea Urusi mashinikizo mapya kwa njia ya vikwazo vya kiuchumi, kisiasa, na kijeshi.

Alisema kuwa Urusi inapaswa kusitisha vita mara moja, akiongeza kuwa endapo hakutakuwa na makubaliano yoyote ya amani ndani ya siku 50 zijazo, Marekani itachukua hatua kali zaidi. Hatua hizo zitajumuisha ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa kutoka Urusi na vikwazo kwa nchi yoyote itakayoshirikiana na Urusi kiuchumi katika mazingira ya vita.