×

Rais Dkt. Samia Azindua Dira Ya Taifa Ya Maendeleo 2050, Dodoma – (Video +Picha)

Dodoma, Julai 17, 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imejenga msingi wa maendeleo kwa kuendeleza juhudi za awamu zilizotangulia na sasa inaweka mkazo katika kuimarisha uchumi jumuishi na shindani unaogusa maisha ya kila Mtanzania.

Akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, iliyofanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Rais Samia alieleza kuwa historia ya maendeleo ya taifa imekuwa ni safu ya hatua thabiti kutoka awamu moja hadi nyingine, kila moja ikiwa na mchango wake wa kipekee.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya heshima na shukrani kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Profesa Kitila Alexander Mkumbo kwenye hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma tarehe 17 Julai, 2025.

“Awamu ya kwanza ilitufundisha kuwa msingi wa Taifa ni utu na usawa. Awamu ya pili ilifungua milango ya uchumi wa soko na demokrasia ya vyama vingi. Awamu ya tatu iliimarisha taasisi za uwajibikaji na utawala bora. Awamu ya nne iliongeza kasi ya maendeleo ya jamii na huduma bora kwa wananchi, ikiwa na kaulimbiu ya ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’. Awamu ya tano ilijikita katika uchumi wa viwanda na miradi mikubwa ya kimkakati ya usafiri na usafirishaji,” alieleza Rais Samia.

Akaongeza kuwa serikali ya sasa imejikita katika kupanua uchumi jumuishi kwa kuwalenga watu wa kada zote, kutoka mijini hadi vijijini, huku ikiendelea kukuza uchumi, kuwezesha wanawake na vijana, na kushirikisha sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Rais Samia akizindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Mantiki ya kuandaa Dira ya miaka 25 ni kuhakikisha kuna uendelevu wa mipango na mikakati ya kuliendeleza Taifa letu,” alisisitiza Rais Samia.

Katika hotuba yake, Rais Samia alibainisha kuwa Dira ya 2050 inalenga kutengeneza mwelekeo wa muda mrefu wenye msingi thabiti wa kisera na kijamii ili kufanikisha maendeleo ya watu wote. Alisisitiza kuwa mafanikio hayatatokana na serikali peke yake bali ni kwa mshikamano wa pamoja kati ya sekta ya umma, binafsi, na wananchi.

Uzinduzi wa Dira ya 2050 unaendelea kuwa hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea maendeleo endelevu, huku msisitizo ukiwekwa kwenye usawa, uwajibikaji, na ushirikishwaji wa wananchi wote.

Rais wa Jamhuri ya Dkt. Samia akionesha nakala za vitabu vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mara baada ya uzinduzi katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma tarehe 17 Julai, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali kwenye hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma tarehe 17 Julai, 2025.