×

Rais Samia Kuzindua Rasmi Dira Ya Maendeleo Ya Taifa 2050

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan

Dodoma, Julai 17, 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Alhamisi amezindua rasmi Dira Mpya ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Hii ni mara ya pili kwa Taifa kuzindua dira ya aina hii, baada ya ile ya mwaka 2025 iliyoasisiwa na Hayati Rais Benjamin William Mkapa mwaka 2000.

Akizungumza katika hafla hiyo ya kihistoria, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema Dira ya 2050 ni ya kipekee kwa kuwa imeandaliwa kwa ushirikishwaji mkubwa wa wananchi. Takribani wananchi milioni 1.17 walifikiwa moja kwa moja, huku wengine zaidi ya 20,000 wakishiriki kupitia makongamano, mikutano ya wadau na njia za kidijitali kupitia tovuti maalum ya Tume ya Taifa ya Mipango.

Prof. Mkumbo alifafanua kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Dira ya Maendeleo imeidhinishwa na Baraza la Mawaziri pamoja na kuridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hatua hiyo inalenga kuipa Dira hiyo hadhi ya kitaifa na kuiweka katika msingi wa utekelezaji endelevu bila kujali mabadiliko ya uongozi wa kisiasa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

“Kwa mara ya pili nchi yetu inazindua Dira ya Maendeleo ya Taifa isiyoegemea itikadi za kisiasa. Rais Samia Suluhu Hassan anakuwa kiongozi wa pili baada ya Hayati Mkapa kuandika dira ya Taifa,” alisema Prof. Kitila.

Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 inalenga kufanikisha ukuaji wa uchumi jumuishi unaopunguza umaskini, kuongeza ajira, kuimarisha mauzo ya bidhaa nje ya nchi, pamoja na kuongeza tija na thamani katika sekta kuu kama vile kilimo, mifugo, madini, na misitu.

Takwimu zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Mipango zinaonyesha kuwa asilimia 81 ya waliochangia maoni kuhusu Dira hii ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35. Hali hiyo inaonesha hamasa ya kizazi kipya kushiriki kikamilifu katika mwelekeo wa maendeleo ya nchi.

Uzinduzi wa Dira ya Taifa ya 2050 unaashiria mwanzo wa safari mpya ya maendeleo ya muda mrefu kwa Tanzania, huku msisitizo ukiwekwa katika ubunifu, usawa, na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.