×

CEO na Afisa Rasilimali Watu Wajiuzulu Baada ya Kuumbuliwa Kwenye Tamasha

Kampuni ya teknolojia ya Astronomer, inayojihusisha na huduma za usimamizi wa data na mfumo wa Apache Airflow, imejikuta katika hali ya sintofahamu baada ya viongozi wake wawili wakuu kuondoka kwa mfululizo, kufuatia video ya utata iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Astronomer, Andy Byron, alijiuzulu rasmi kufuatia uchunguzi wa ndani ulioanzishwa na kampuni hiyo. Uchunguzi huo ulitokana na video iliyopigwa kwenye tamasha la muziki la Coldplay, ambayo ilimuonesha Byron akiwa katika hali ya karibu mno na mfanyakazi mwenzake, Kristin Cabot, ambaye alikuwa Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu (CHRO) wa kampuni hiyo.

Katika video hiyo, wawili hao walionekana wakiwa wamekumbatiana kimahaba mbele ya hadhira kubwa, huku sura zao zikionyeshwa kwenye skrini kubwa ya jukwaani. Baada ya kugundua kuwa wamekuwa sehemu ya matangazo ya moja kwa moja kwenye skrini hiyo, walionekana wakijificha kwa ghafla—kitendo kilichozua gumzo kubwa mtandaoni.

Cabot Naye Aondoka Astronomer

Baada ya video hiyo kusambaa na kusababisha hali ya taharuki ndani ya kampuni, Astronomer imethibitisha kwamba Kristin Cabot naye ameondoka rasmi. Taarifa ya kampuni ilisema kwa kifupi:

“Kristin Cabot hafanyi tena kazi na Astronomer.”

Hii ni hatua iliyotafsiriwa na wachambuzi kama jaribio la kampuni kuokoa taswira yake mbele ya wafanyakazi na umma, huku maswali mengi yakiibuliwa kuhusu maadili ya viongozi, matumizi ya madaraka, na mazingira ya kazi.

Kwa sasa, bado haijafahamika rasmi ni nani atakayechukua nafasi ya Byron au Cabot katika kampuni hiyo.

MASHABIKI wa SIMBA WACHARUKA na KUUWASHIA MOTO UONGOZI WAO – “HATUJAPATA UBINGWA MIAKAMINNE”…