
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania imefanikiwa kuendesha Uchaguzi wa saba wa kidemokrasia tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo wakati akihutubia hafla ya kufungua mwaka mpya wa 2026, iliyowakutanisha Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania, wawakilishi wa heshima pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino.
Amesema Uchaguzi huo ulifadhiliwa kikamilifu kwa kutumia rasilimali za ndani, hatua inayodhihirisha umiliki wa kitaifa, ukomavu wa taasisi za nchi pamoja na dhamira ya Serikali ya kujitegemea katika kusimamia na kuimarisha mchakato wa kidemokrasia.

Hata hivyo, Rais Samia amekiri kuwepo kwa changamoto zilizojitokeza siku ya uchaguzi na muda mfupi baada ya zoezi hilo, hususan vurugu na hali ya kutokuwepo kwa utulivu katika baadhi ya maeneo.
“Licha ya mafanikio haya makubwa, kwa masikitiko tunatambua changamoto zilizotokea kutokana na vurugu na ukosefu wa utulivu siku ya uchaguzi na muda mfupi baada yake. Hatua tulizochukua zilikuwa muhimu ili kudumisha utaratibu wa Kikatiba na kuhakikisha usalama wa wananchi wote pamoja na Jamii ya Kidiplomasia,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia aliwapa pole Washirika wa Kidiplomasia na wageni wanaoishi nchini kutokana na changamoto walizokumbana nazo, ikiwemo usumbufu wa huduma na kufungwa kwa mtandao wa intaneti.
“Kwa Washirika wetu katika Jamii ya Kidiplomasia na wageni wanaoishi hapa nchini Tanzania, ninatoa pole ya dhati kutokana na hali ya kutokuwa na uhakika, usumbufu wa huduma, na kufungwa kwa mtandao wa intaneti. Nawaahidi kuwa tutakuwa makini kuhakikisha usalama wenu na kuzuia hali kama hiyo kujirudia katika siku zijazo,” aliongeza.