
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema anaamini kuwa China imekuwa na mchango mkubwa katika kuishawishi Iran kukubali kuingia kwenye mazungumzo ya kusitisha vita dhidi ya Marekani na Israel.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Trump alidai kuwa juhudi za China zimechangia kufikiwa kwa hatua ya mazungumzo, wakati mvutano wa kijeshi ukiendelea kuitikisa dunia.
Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilikaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano, ikisisitiza kuwa nchi hiyo imekuwa ikihimiza mara kwa mara suluhisho la kidiplomasia badala ya vita. Msemaji wa wizara hiyo, Mao Ning, alisema China imekuwa ikitaka kusitishwa kwa mapigano mara moja na migogoro kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo ya kisiasa.
Hata hivyo, China haikutoa maelezo ya kina kuhusu namna ilivyohusika moja kwa moja katika kufanikisha mazungumzo hayo.
Katika hatua nyingine, Trump alithibitisha kusimamisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran kwa muda wa wiki mbili, akieleza kuwa uamuzi huo umetokana na mazungumzo yake na viongozi wa Pakistan, akiwemo Waziri Mkuu Shehbaz Sharif pamoja na mkuu wa jeshi, Jenerali Asim Munir.
Masharti ya kusitishwa kwa mashambulizi hayo yanahusisha kufunguliwa kwa njia muhimu ya usafirishaji mafuta duniani, Strait of Hormuz, ambayo imekuwa chanzo kikubwa cha mvutano tangu kuanza kwa vita hiyo Februari 28.
Trump alisema Marekani imepokea pendekezo la vipengele 10 kutoka Iran, ambavyo vinaweza kuwa msingi wa kufikia makubaliano ya kudumu. Aliongeza kuwa mambo mengi yaliyokuwa yakizua mgogoro tayari yamefikiwa muafaka, huku kipindi cha wiki mbili kikitarajiwa kukamilisha makubaliano hayo.
Vita hiyo iliyoanza baada ya mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran imeacha maelfu ya watu wakiwa wamefariki na mamilioni wakikimbia makazi yao, huku pia ikitikisa uchumi wa dunia na kupandisha bei ya mafuta.
Licha ya hatua hiyo ya kusitisha mashambulizi, hali bado inaendelea kuwa tete, huku macho ya dunia yakielekezwa kwenye mazungumzo yajayo yatakayoamua hatma ya mzozo huo mkubwa wa kimataifa.