
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Marekani haihitaji makubaliano ya kidiplomasia na Iran ili kupata uranium iliyorutubishwa kutoka nchini humo, akitoa kauli inayoendelea kuzua mjadala kuhusu uhusiano wa mataifa hayo mawili.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya White House, Trump alisema Marekani inaweza kuipata sasa hivi na kuongeza kuwa hakuna anayeweza kuizuia ikiwa ingeamua kufanya hivyo, ingawa hakufafanua kwa undani njia ambayo angeitumia.

“Tunaiweza kupata sasa hivi. Sidhani kama wanaweza kutuzuia kama tungetaka, lakini hakuna sababu ya kufanya hivyo. Imefichwa,” alisema Trump.
Katika kauli hiyo, Trump pia alisema hataki kukutana na Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, lakini akaongeza kuwa endapo makubaliano yatapatikana kati ya Washington na Tehran, anaweza kukutana naye kwa heshima.
“Kama ikitokea, nitaheshimu hilo” aliongeza.
Kauli hiyo inakuja wakati ambapo mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea, huku juhudi za kidiplomasia zikijaribu kutafuta suluhu kuhusu suala la nyuklia na usalama wa kikanda.