
WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amewaalika wafanyabiashara kutoka Ufaransa waje kuwekeza nchini Tanzania kwani ina fursa ya kutengeneza ajira, kuhamisha ujuzi na kujenga uchumi wa viwanda kwa faida ya nchi zote mbili.
“Leo tumefanya mjadala wa kibiashara na sote tumeshuhudia makubaliano yakisainiwa baina ya Tanzania Private Sector Foundation na International Chamber of Commerce (ICC). Makubaliano haya siyo tu mkataba wa kawaida bali ni daraja la kutupeleka kwenye mafanikio makubwa huko mbele,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo Jumatatu, Julai 6, 2026 wakati akizungumza na washiriki wa mjadala wa kibiashara baina ya Tanzania na Ufaransa (Tanzania-France Business Roundtable) uliofanyika kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania jijini Paris, Ufaransa.

“Kwa hiyo ninawahimiza wafanyabiashara wa Ufaransa mtumie vyema fursa hii ya kipekee. Maamuzi yatakayofanywa leo ndiyo yatakayoamua mwelekeo wa sekta za uchumi za kesho kwa nchi zetu. Wale watakaowekeza nchini Tanzania hivi sasa, hawatakuwa tu sehemu ya mageuzi ya uchumi wetu, bali watakuwa washirika wa thamani katika kujenga moja ya uchumi wenye ushindani mkubwa zaidi barani Afrika kwa vizazi vijavyo.”
Dkt. Mwigulu amesema Ufaransa inao utaalamu wa hali ya juu na wa kiwango cha kimataifa katika teknolojia, uhandisi, nishati, miundombinu, viwanda, masuala ya fedha, na huduma za afya.

Waziri Mkuu pia alishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Chama cha Kimataifa cha Biashara cha Ufanransa (ICC) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), ambapo Mtendaji Mkuu wa TPSF, Bw. Deo Massawe alibadilishana hati hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa ICC, Bw. Julia Kassum.
Baadhi ya kampuni za Ufaransa zilizoshiriki mjadala huo zinajihusisha na usimamizi wa nishati ya jua (ikiwemo mifumo ya taa za barabarani), usafirishaji, maji, nishati, ujenzi, viwanda, mazingira na ufugaji wa viumbe maji (ikiwemo uzalishaji wa mwani wa baharini). Kampuni nyingine ni waendeshaji wa huduma za satelaiti wanaotoa suluhisho bunifu kwa huduma za utangazaji wa sauti na picha, intaneti ya kasi (broadband), huduma za data, usafiri wa baharini na anga.
