×

Kim Kardashian Avamiwa Nyumbani, Mtu Mmoja Akamatwa

Nyota wa Marekani Kim Kardashian amekumbwa na tukio la uvamizi katika moja ya nyumba zake zilizopo eneo la Hidden Hills, Los Angeles, ambapo mwanaume mwenye umri wa miaka 27 amekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.

Kwa mujibu wa mamlaka, tukio hilo lilitokea Jumapili, Agosti 9, 2026, baada ya mlinzi wa usalama kutoa taarifa kuhusu mtu aliyeingia katika eneo la nyumba hiyo.

Maafisa wa Los Angeles County Sheriff’s Department walifika katika eneo hilo na kumkamata mtuhumiwa kwa tuhuma za uvamizi.

Taarifa zinaeleza kuwa mtuhumiwa aliingia katika eneo hilo kupitia mlango wa pembeni na baadaye alionekana akipakia baadhi ya vitu kwenye gari. Pia anadaiwa kuchukua gari lililokuwa katika eneo hilo na kulitumia kabla ya kukamatwa. Gari hilo limeripotiwa kuwa la mfanyakazi, si la Kardashian mwenyewe.

Wakati tukio hilo likitokea, Kardashian na watoto wake hawakuwa katika nyumba hiyo. Nyumba hiyo kwa sasa haikaliwi na familia hiyo kutokana na kuendelea kwa shughuli za ukarabati. Hakuna taarifa za mtu yeyote kujeruhiwa katika tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea.

Nyumba hiyo ya kifahari iliyopo Hidden Hills imewahi kuripotiwa kuwa na thamani ya takribani dola milioni 60 za Marekani. Kardashian aliinunua pamoja na aliyekuwa mume wake, Kanye West, mwaka 2014, kabla ya baadaye kubaki na umiliki wa mali hiyo baada ya talaka yao.

Tukio hilo linarejesha kumbukumbu ya tukio jingine kubwa la kiusalama lililompata Kardashian mwaka 2016, alipovamiwa kwa kutumia silaha akiwa Paris, Ufaransa, na kuibiwa vito vya thamani. Tukio hilo lilimwathiri kwa kiasi kikubwa na kumfanya kuongeza zaidi hatua za usalama katika maisha yake.

 

Leave a Comment