
Shahidi wa Tatu wa utetezi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Amani Sam Golugwa leo Septemba 2, 2026 amepanda kizimbani na kuanza kutoa ushahidi wake, akieleza kuhusu nafasi yake ndani ya Chadema, maandalizi ya mkutano wa watia nia na chanzo cha msimamo wa chama wa “No Reform, No Election.”
Golugwa, mwenye umri wa miaka 49 na anayeishi Goba, amejitambulisha mahakamani kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, nafasi ambayo amesema ameishikilia tangu Januari 22, 2025.
Kabla ya nafasi hiyo, amesema aliwahi kuwa Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini kuanzia Februari 2013, akisimamia mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Amesema pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha kuanzia mwaka 2014 hadi 2019, huku kati ya mwaka 2008 na 2014 akiwa Katibu wa chama hicho mkoani Arusha.
Golugwa ameieleza Mahakama kuwa mwaka 2020 aliteuliwa na Chadema kuwa Kampeni Meneja wa aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho, Tundu Lissu, na kwamba wakati huo alikuwa akijulikana kwa jina la “Mnikulu.”
Amesema amekuwa mwanachama wa Chadema tangu mwaka 2007.
Aeleza namna alivyopata nafasi ya Naibu Katibu Mkuu
Akijibu swali la Lissu kuhusu namna mtu anavyopata nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Golugwa amesema jina la mgombea hupendekezwa na Mwenyekiti wa chama na kuwasilishwa mbele ya Baraza Kuu kwa ajili ya kuthibitishwa.
Amesema majukumu yake kama Naibu Katibu Mkuu ni pamoja na kuwa msaidizi wa Katibu Mkuu, kuandika kumbukumbu za vikao vya chama na kusimamia itifaki katika vikao na mikutano ya chama.
Kitaaluma, Golugwa amesema amesomea Uhasibu katika Chuo cha Uhasibu Arusha hadi ngazi ya Post Graduate Diploma in Accountancy.
Amesema alianza kufanya kazi katika eneo la uhasibu mwaka 2001 kama Accounts Assistant na aliendelea na kazi hiyo hadi mwaka 2015.
Aeleza maandalizi ya mkutano wa Aprili 3, 2025
Akianza kuelezea mazingira ya kesi, Golugwa amesema anaifahamu mikutano ambayo inahusishwa na tuhuma zinazomkabili Lissu.
Amesema mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025 uliandaliwa na Sekretarieti ya Chadema baada ya Katibu Mkuu kuwasilisha wazo la kuwakutanisha watia nia wa chama.
Kwa mujibu wa Golugwa, Sekretarieti ya Chadema inajumuisha Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Wakuu wawili wa Zanzibar na Bara, makatibu wa mabaraza ya wanawake, vijana na wazee, wakurugenzi pamoja na wataalamu walioteuliwa na Mwenyekiti.
Amesema jumla ya watu wanaounda Sekretarieti hiyo ni 14, na kwamba ni chombo cha kiutendaji kinachoshughulikia shughuli za kila siku za chama kwa niaba ya Kamati Kuu.
Akifafanua maana ya “watia nia”, Golugwa amesema walikuwa wanachama wa Chadema waliokuwa na nia ya kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais katika uchaguzi wa mwaka 2025.
Amesema baadhi yao waliwahi kupitishwa kuwa wagombea katika uchaguzi wa 2020, huku wengine wakiwa hawajawahi kugombea nafasi hizo.
“No Reform, No Election”
Golugwa amesema lengo kubwa la mkutano huo lilikuwa kuwaeleza watia nia msimamo wa Chadema uliopitishwa na Mkutano Mkuu na kufafanuliwa na Kamati Kuu kuhusu kauli ya “No Reform, No Election.”
Ameeleza kuwa msimamo huo ulianza baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024.
Kwa mujibu wa Golugwa, akiwa Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Katibu Mkuu aliwataka makatibu wa kanda kuandaa ripoti kuhusu namna uchaguzi huo ulivyofanyika.
Amesema ripoti yake ilieleza kile alichodai kuwa ni ukiukwaji na matatizo mbalimbali aliyoyaona wakati wa uchaguzi huo.
Golugwa ameliambia Mahakama kuwa katika ripoti yake alitumia lugha kali na kupendekeza Chadema ishiriki katika uchaguzi mwingine bila kwanza kushinikiza mabadiliko ya uchaguzi.
Amesema makatibu wengine wa kanda pia waliwasilisha mapendekezo yaliyokuwa na mwelekeo unaofanana.
Baada ya mapendekezo hayo kufanyiwa kazi, amesema Kamati Kuu ya Chadema ilijadili suala hilo na baadaye, Desemba 10, Mwenyekiti wa chama wakati huo, Freeman Mbowe, akatoa tamko rasmi.
Kwa mujibu wa Golugwa, msimamo wa Kamati Kuu ulikuwa kwamba Chadema haitakuwa tayari kushiriki uchaguzi mwingine bila kufanyika mabadiliko ya Kikatiba na kisheria, ndipo kauli ya “No Reform, No Election” ikatumika.
Ushahidi wa Golugwa unaendelea mbele ya Mahakama huku upande wa utetezi ukiendelea kueleza mazingira yaliyopelekea Chadema kuchukua msimamo huo kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025.
Unaitwa Nani?
Amani Sam Golugwa.
Una miaka mingapi: 49
Unaishi wapi: Goba
Kazi yako?
Mimi ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara.
Dini yako?
Mkristo.
Sasa fanya kuapa hapo.
Anaapa, Mimi Amani Golugwa naapa nitatoa ushahidi wa kweli na Mungu unisaidie.
Anashusha chini Biblia.
Lissu: Sasa umesema wewe ni Naibu Bara umeishikilia toka lini?
Golugwa: Nimekuwa Naibu Katibu Mkuu toka January 22, 2025.
Lissu: Kabla ya nafasi hiyo ulikuwa na nafasi gani kwenye Chama?
Golugwa: Nimekuwa Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini toka mwaka 2013 mwezi wa 02
Lissu: Katibu wa Kanda ya Kaskazini una maana gani?
Golugwa: Namaanisha Mikoa minne. Tanga, Arusha, Kilimanjaro. Manyara. Na hiyo ndio Kanda ya Kaskazini.
Lissu: Kabla ya hapo ulikuwa na nafasi gani?
Golugwa: Nimeshika nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha kutoka 2014 hadi 2019.Kutoka 2008 hadi 2014 nilikuwa Katibu wa Mkoa wa Chadema. Huko Arusha.
Lissu: Kama kuna nafasi nyingine uliwahi kuishikilia nje ya hizo?
Golugwa: Mwaka 2020 niliteuliwa na Chama kuwa Kampeni Manager wa aliyekuwa mgombea wa Urais kupitia tiketi ya Chadema Mh. Tundu Lissu.
Lissu: Walikuwa wanakuita Mnikulu?
Golugwa: Sahihi.
Lissu: Umeingia Chama hiki lini?
Golugwa: Toka 2007 hadi leo nimekuwa Mwanachama wa CHADEMA. Takribani miaka 19.
Lissu: Mtu anapataje nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara?
Golugwa: Ili mtu awe Naibu Katibu Mkuu jina lake litapendekezwa na Mwenyekiti wa Chama kwa maana atatafuta mwanachama mwenye uwezo atapendekeza mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Chama na Katiba yetu imeelekeza atapeleka jina moja aliloliteua kwa wanachama wengi na wajumbe wa Baraza Kuu watafanya wajibu wa kuthibitisha kwa huyo aliyependekezwa.
Lissu: Majukumu ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema ni
1. msaidizi wa Katibu Mkuu. Anamsaidia Katibu Mkuu.
2. Mwandishi wa Kumbukumbu za Vikao vya Chama.
3. Amepewa nafasi kwamba ndie mkuu na msimamizi wa Itifaki katika vikao na mikutano ya Chama.
Lissu: Waeleze majaji wasifu wako wa kitaaluma?
Golugwa: Elimu ya Chuo nimesoma masuala ya Uhasibu. Nimesoma uhasibu chuo cha Uhasibu Arusha hadi ngazi ya stashada ya uzamili yaani Post Graduate Diploma in Accountancy.
Lissu: Uzoefu wako katika eneo hilo la Uhasibu?
Golugwa: Nimefanya kazi ya Uhasibu nikianza ngazi ya Accounts Assistant na kufanya kazi ya Uhasibu hadi mwaka 2015. Toka mwaka 2001 kwenye maeneo tofauti tofauti.
Lissu: Sasa tuzungumze hii kesi. Wanasema nilitoa maneno ya kuitishia serikali ya Jamhuri ya Muungano na kukinukisha?
Golugwa: Huo Mkutano nina ufahamu.
Lissu: Waeleze Majaji Mkutano uliandaliwa na nani na ulifanyikia wapi?
Golugwa: Huu Mkutano uliandaliwa na Sekretarieti ya Chama baada ya Katibu Mkuu kuleta wazo kwenye sekretarieti kwamba watia nia ni wadau muhimu hivyo tuandae Mkutano wa kukutana na watia nini?
Sekretarieti ilifanya maandalizi yote ya Mkutano.
Lissu: Sekretarieti ni akina nani?
Golugwa: Hii sekretarieti ninayozungumzia ni
1. Katibu Mkuu wa Chama,
2. Manaibu wawili wa Zanzibar na Bara,
3. Makatibu wa Mabaraza ya Chama yaani Wanawake, Vijana na Wazeee.
4. Wakurugenzi wa Chama
5. Pamoja na Wataalamu wa Chama ambao wameteuliwa na Mwenyekiti kuwa Sekretarieti ya Chama.
Lissu: Jumla ni watu wangapi?
Golugwa: Ni watu 14.
Lissu: Sekretarieti ni Chombo cha aina gani kwa muundo wa Chadema?
Golugwa: Sekretarieti ya Chadema ndicho chombo cha kiutendaji kinachofanya kazi za kila siku za Chama kwa niaba ya Kamati Kuu ya Chama.
Lissu: Sasa unasema kwamba Katibu Mkuu alikuja na wazo la kwamba muandae mkutano wa wadau muhimu, watia nia.
Watia nia ni akina nani?
Amani Sam Golugwa: Waheshimiwa Majaji, watia nia ni wanachama wa CHADEMA ambao aidha walipitishwa na kuwa wagombea kwenye uchaguzi wa 2020 katika nafasi za udiwani, ubunge na urais, na kwamba bado nia yao ya kutaka kugombea nafasi hizo bado walikuwa nayo.
Na wengine katika kundi hilo la watia nia ni wale ambao hawajawahi kupitishwa wala kugombea nafasi hizo nilizotaja (fresh kabisa).
Na hivyo, 2025 walikuwa na nia na wao wagombee kupitia CHADEMA, waombe nafasi ndani ya Chama na wapitishwe kuwa wagombea wa ubunge, udiwani na urais.
Hao ndiyo watia nia.
Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji hao watia nia walikuwa na nia ya kugombea uchaguzi gani?
Amani Sam Golugwa: Waheshimiwa Majaji, hawa watia nia walikuwa na nia ya kugombea katika uchaguzi wa 2025.
Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, lengo la kuwaita hao watia nia kuja katika mkutano wa tarehe 3 Aprili 2025 lilikuwa ni lengo gani?
Amani Sam Golugwa: Lengo lilikuwa ni kuwaeleza na kuwafafanulia juu ya msimamo wa Chama uliopitishwa na Mkutano Mkuu, kwa maana ya wazo la “No Reform, No Election”, na msimamo huo ukawa umefafanuliwa na Kamati Kuu ya Chama kwa kuazimiwa.
Hilo ndiyo lilikuwa lengo la kuwaeleza na kuwafafanulia lengo na “No Reform, No Election.”
Lissu: Huu msimamo wa “No Reform, No Election” ulikuwa unahusu nini hasa? Naomba ufafanuzi.
Amani Sam Golugwa: Msimamo huu ulianza au ulizaliwa baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Nikiwa Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Katibu Mkuu alituambia makatibu wa kanda tuandike ripoti ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa jinsi ulivyofanyika.
Na mimi kama mtendaji ambaye nilikuwa sehemu ya uchaguzi huo, kwa kusimamia Kanda ya Kaskazini, nilitoa ripoti yenye kuonyesha madudu mengi ya ovyo yaliyojitokeza.
Na Katibu Mkuu alitutaka makatibu wa kanda tuandike maoni yetu kuhusiana na yaliyotokea ambayo tuliona ya ovyo yaliyojitokeza.
Mimi kwenye ripoti niliandika:
“Naomba Waheshimiwa Majaji niseme katika ripoti niliyomtumia Katibu Mkuu nilitumia maneno makali.
Niliandika hivi:
‘Kwa ushenzi huu nilioona, Chama kisishiriki uchaguzi mwingine wowote, uchaguzi mwingine wowote, bila kushinikiza mabadiliko ya kiuchaguzi.’”
Mimi na makatibu wenzangu, kila mmoja kwa lugha yake, tulitoa pendekezo linalofanana.
Nikachakata mapendekezo ya makatibu wa kanda, na wajumbe wenyewe wa Kamati Kuu wakajadili na kutafakari kwa jinsi wanavyojua.
Nasi tarehe 10 mwezi wa Desemba, Mwenyekiti wa Chama kipindi hicho, Mheshimiwa Freeman Mbowe, akatoa tamko rasmi la Chama.
Msimamo wa Kamati Kuu uliazimiwa kwamba hatutakuwa tayari kwenda kwenye uchaguzi mwingine wowote bila ya mabadiliko ya Kikatiba na kisheria.
Akasema kwa Kiingereza, “No Reform, No Election.” Kesi inaendelea.