Ikulu imeonya umma dhidi ya kusambaza taarifa za uongo zinazohusu shughuli za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, zikieleza kuwa taarifa rasmi hutolewa kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Katika taarifa iliyotolewa Zanzibar leo, Septemba 8, 2026, Kurugenzi hiyo imesema imebaini uwepo wa taarifa zinazotengenezwa kwa sura ya taarifa rasmi na kusambazwa mitandaoni zikidaiwa kutoka Ikulu au kuhusishwa na Rais.
Ikulu imesema taarifa zote rasmi kuhusu shughuli za Rais hutolewa kupitia tovuti na kurasa rasmi za Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ikiwemo Instagram @ikulu_mawasiliano, Facebook @ikulu.mawasiliano pamoja na tovuti ya Ikulu.
Kurugenzi hiyo imesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuthibitisha taarifa kuhusu Rais kupitia vyanzo rasmi kabla ya kuzipokea au kuzisambaza, ili kuepuka kueneza taarifa za upotoshaji.
Aidha, Ikulu imekumbusha kuwa utengenezaji na usambazaji wa taarifa za uongo kwa kutumia jina, nembo au utambulisho wa Rais bila ruhusa ni kosa kwa mujibu wa Vifungu vya 15 na 16 vya Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sura ya 443.
Taarifa hiyo imesainiwa na Bakari S. Machumu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

