×

Ndejembi Aongoza Maandalizi ya Tanzania katika Jukwaa la IAEA Vienna


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameongoza kikao cha maandalizi cha viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka Tanzania wanaoshiriki Jukwaa la Kisayansi la Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA Scientific Forum), mara baada ya kuwasili Vienna, Austria leo Septemba 14, 2026.

Ndejembi anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Jukwaa hilo la Kisayansi litakalofanyika Septemba 15 na 16, 2026, jijini Vienna, Austria.

Jukwaa hilo linafanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa 70 wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (International Atomic Energy Agency – IAEA), unaowakutanisha viongozi, wataalamu na wadau mbalimbali kujadili masuala yanayohusu matumizi salama na yenye manufaa ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.

Ushiriki wa Tanzania katika mikutano hiyo unalenga kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo ya taifa, hususan katika sekta muhimu za afya, kilimo, nishati, maji na mazingira.

Leave a Comment