
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa athari zinazohusishwa na hali ya El Niño katika kipindi cha mvua za Vuli za miezi ya Oktoba hadi Desemba 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo, tarehe 18 Agosti 2026, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba–Desemba 2026), ambao unaashiria kuwepo kwa viwango vikubwa vya hali ya El Niño kwenye eneo kubwa la Bahari ya Pasifiki.
Hali hiyo inatarajiwa kuchangia ongezeko la mvua za Vuli za mwaka 2026 kuwa juu ya wastani katika baadhi ya maeneo nchini.
Wizara imesema baadhi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali hiyo ni pamoja na mafuriko, maporomoko ya ardhi, kujaa kwa mito na mifereji, uharibifu wa miundombinu ya barabara, reli, madaraja na majengo, pamoja na uharibifu wa mali na mazao.
Aidha, imeonya kuwa kuna uwezekano wa kuongezeka kwa hatari ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama.
Kutokana na hali hiyo, Wizara imetoa wito kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.
Maafisa hao wametakiwa pia kuwatambua wananchi walio katika mazingira hatarishi, hususan watoto, wazee na watu wenye ulemavu, pamoja na kufanya maandalizi ya utoaji wa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa wananchi watakaoathiriwa na mvua hizo.
Kwa upande wa wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla, Wizara imewataka kuchukua tahadhari mapema kwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa, kuepuka kuvuka mito au maeneo yaliyofunikwa na maji na kutoa usaidizi kwa watu wenye ulemavu na wazee wasiojiweza.
Wananchi pia wametakiwa kutoruhusu watoto kucheza karibu na mifereji, mitaro, mito, makalavati, madaraja na maeneo ambayo maji yanapita kwa kasi.
Aidha, wametakiwa kusafisha mitaro na mifereji ya kupitisha maji ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, pamoja na kuhakikisha wanapata maji salama ya kunywa na kupikia wakati wote.
Wizara imewataka pia wakazi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni, karibu na mito na maeneo yenye historia ya mafuriko au maporomoko ya ardhi kuwa waangalifu zaidi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, ikiwemo kuhama mapema endapo wataelekezwa kufanya hivyo.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Charles F. Komba, Septemba 19, 2026.
