Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameondoka nchini leo Jumamosi, Septemba 19, 2026, kuelekea Roma, Italia, kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Kimataifa wa Afya Moja (One Health) na Mifumo ya Chakula na Kilimo.
Mkutano huo utafanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, kuanzia Septemba 21 hadi 23, 2026.
Mkutano huo unalenga kuimarisha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, inayotambua uhusiano uliopo kati ya afya ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira, kwa lengo la kujenga mifumo endelevu ya chakula na kilimo.

Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi na Serikali, wakiwemo Marais kati ya watano hadi saba, Mawaziri kati ya 30 hadi 50, pamoja na wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa, wadau wa maendeleo, sekta binafsi, taasisi za utafiti na mashirika ya kimataifa.
Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni namna ya kuingiza dhana ya Afya Moja katika sera na uwekezaji wa mifumo ya chakula na kilimo, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za kilimo, mazingira, afya, fedha na mipango miji.
Aidha, mkutano huo utajadili ukuzaji wa ubunifu, sayansi na maarifa ya ndani kwa ajili ya kuboresha uzuiaji wa vihatarishi, ufuatiliaji na usimamizi endelevu wa rasilimali.
Pia, washiriki watajadili namna ya kuhamasisha uwekezaji na ushirikiano ili kutafsiri ahadi zilizotolewa kuwa hatua madhubuti zenye matokeo yanayoweza kupimika.
