
Serikali imewaagiza watumishi wa umma na taasisi za Serikali zilizokuwa zimepanga katika majengo mengine ya umma kuyaachia na kurejea katika majengo yao yaliyopo Mji wa Serikali , jijini Dodoma, baada ya kukamilika kwa ujenzi wake.
Agizo hilo limetolewa Jumanne, Oktoba 28, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akitoa taarifa kuhusu uzinduzi rasmi wa Mji wa Serikali Mtumba unaotarajiwa kufanyika Oktoba 30, 2026.
Profesa Kabudi amesema baadhi ya taasisi za Serikali zililazimika kutumia majengo mengine, yakiwemo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kufuatia uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma, lakini kwa sasa majengo yao yamekamilika na hivyo wanapaswa kurejea katika maeneo yao rasmi ya kazi.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha taasisi za Serikali zinafanya kazi katika majengo yaliyotengwa kwa ajili yake ndani ya Mji wa Serikali Mtumba.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, wazo la kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma lilitolewa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1973, huku utekelezaji wa uhamisho huo ukiendelea kwa awamu mbalimbali.
Ameeleza kuwa kasi ya kuhamia Dodoma iliongezeka wakati wa Awamu ya Tano, hatua iliyokwenda sambamba na kutungwa kwa sheria rasmi ya kuitambua Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.
Akizungumzia gharama za ujenzi, Profesa Kabudi amesema ujenzi wa awamu ya kwanza ulianza Novemba 28, 2018, na kugharimu Sh39.39 bilioni.
Ameongeza kuwa ujenzi wa awamu ya pili umefikia zaidi ya asilimia 99 ya utekelezaji, huku gharama zake zikifikia zaidi ya Sh940.8 bilioni.
“Leo majengo yamefikia zaidi ya asilimia 99 baada ya kutumia zaidi ya Sh940.8 bilioni kwenye awamu ya pili, sasa ni muda muafaka watumishi kuachia majengo yale na kwenda Mtumba,” amesema Profesa Kabudi.
Amesema uzinduzi huo utahusisha majengo 37 yaliyopo ndani ya Mji wa Serikali Mtumba pamoja na majengo mengine 35 yaliyojengwa nje ya eneo kuu la mji huo.
Aidha, amesema ujenzi wa miundombinu ya barabara zenye urefu wa kilomita 57.1 umekamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh110.5 bilioni.
Uzinduzi rasmi wa Mji wa Serikali Mtumba utafanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, Oktoba 30, 2026, ikiwa ni hatua nyingine katika utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuimarisha shughuli za utawala na utendaji wa taasisi zake katika makao makuu ya nchi, Dodoma.