×

DPP Kukata Rufaa Dhidi ya Lissu, Mwanasheria wa Chadema Afunguka

Makili wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, wamesema wamejipanga kukabiliana na hatua ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukata rufaa dhidi ya sehemu ya hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru Lissu katika shtaka la uhaini.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, amesema tayari wamepokea taarifa rasmi ya kusudio la DPP kukata rufaa na kwamba wanaendelea na maandalizi ya kisheria ili kujibu hatua hiyo.

Dkt. Nshala amesema maandalizi hayo yanahusisha kupitia kumbukumbu za mwenendo wa kesi pamoja na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu, akisisitiza kuwa kukata rufaa ni haki ya kisheria inayotumiwa na upande wowote usioridhishwa na uamuzi wa mahakama.

Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala.

Hatua ya DPP imekuja baada ya kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, akipinga sehemu ya hukumu iliyotolewa Novemba 6, 2026, katika Kesi ya Jinai Namba 19605 ya mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyopokelewa na kusajiliwa Novemba 13, 2026, DPP hajakubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu uliomwachia huru Lissu katika shtaka la uhaini, huku akibainisha kuwa rufaa hiyo inalenga kupinga matokeo ya uchunguzi wa mahakama na amri ya kumuachia huru katika shtaka hilo.

Katika hukumu hiyo, jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, lilimwachia huru Lissu katika shtaka la uhaini, lakini likamkuta na hatia ya kosa la uchochezi wa kutenda kosa chini ya kifungu cha 390 cha Kanuni ya Adhabu na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela.

DPP amewasilisha taarifa hiyo chini ya Kanuni ya 68(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za mwaka 2009, huku akiiomba Mahakama ya Rufani kumpatia nakala ya hukumu na mwenendo wa shauri hilo ili kukamilisha taratibu za rufaa.

Kwa upande mwingine, hatua ya DPP inafuatia taarifa ya kusudio la kukata rufaa iliyowasilishwa na upande wa utetezi wa Lissu Novemba 7, 2026, ukiwa unapinga kutiwa kwake hatiani katika kosa la uchochezi pamoja na adhabu ya kifungo cha miaka minne jela.

Hivyo, pande zote mbili sasa zimeonesha nia ya kupinga sehemu tofauti za hukumu hiyo, huku hatua zinazofuata za kisheria zikitarajiwa kuamua hatma ya malalamiko yao katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Leave a Comment