×

Nahodha wa Mv Mwanza Asimamishwa Kazi Baada ya Ajali ya Meli Kugonga Mwamba – Video

Nahodha aliyekuwa akiendesha meli ya MV Mwanza wakati ilipogonga mwamba katika Ziwa Victoria amesimamishwa kazi mara moja, huku Serikali ikielekeza achukuliwe hatua za kiutawala na kinidhamu kufuatia ajali hiyo.

Hatua hiyo imetangazwa na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, Novemba 26, 2026, akisema uchunguzi wa awali umeonesha kuwa ajali hiyo ilisababishwa na makosa ya kibinadamu (Human Error).

Akizungumza na waandishi wa habari, Prof. Mbarawa alisema Serikali imeelekeza hatua mbalimbali za kiufundi na kiutawala kuchukuliwa ili kuimarisha usalama wa usafiri wa majini na kuzuia matukio kama hayo kujirudia.

Aidha, Waziri huyo ameliagiza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kufanya ukaguzi wa kina wa MV Mwanza na mifumo yake ya uendeshaji pamoja na vifaa vya usalama kabla ya kuruhusu meli hiyo kurejea kutoa huduma.

Alisisitiza kuwa MV Mwanza haitaanza tena safari za kutoa huduma kwa wananchi hadi TASAC itakapojiridhisha kuwa meli hiyo inakidhi viwango vyote vya usalama vinavyotakiwa.

Kwa upande mwingine, Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (TASHICO) imeelekezwa kufanya matengenezo ya eneo la mbele la meli lililoharibika kutokana na ajali hiyo.

Prof. Mbarawa pia ameitaka TASAC kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maagizo hayo na kuhakikisha watumishi wanaohusika na uendeshaji wa meli wana taaluma, ujuzi na uwezo unaostahili kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viwango vya usalama.

Akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika usafiri wa majini, Waziri huyo amesema usalama wa meli, abiria na wafanyakazi unategemea kwa kiasi kikubwa nidhamu na maamuzi sahihi ya nahodha wakati wa kuendesha chombo hicho.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu usalama wa usafiri wa majini kwa kuhakikisha meli zote zinazotoa huduma kwa wananchi zinakidhi matakwa na viwango vinavyotakiwa kabla ya kuruhusiwa kufanya safari.

Leave a Comment