The House of Favourite Newspapers

Heri Ya Mwaka Mpya, TFF Suala La Mdhamini Mlitafutie Ufumbuzi

NINA kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa afya aliyonijaalia na kuweza kunipa kiba­li cha kuuona mwaka 2019, hivyo ninaamini nawe msomaji wangu umefika salama, hivyo tuun­gane kumshukuru.

Siku zote ulikuwa pamoja nami ukisoma busara zangu wakati mwingine nilikukwaza kutokana na ukweli niliokuwa nauandika na wakati mwingine nilikufurahisha kwa kile nili­chokiandika.

 

Asante kwa ushauri na kuwa pamo­ja nami siku zote katika safu hii, hivyo nami nitaendelea kuwa nawe kila siku kwa mapenzi yake anayetupa uhai. Heri ya Mwaka Mpya 2019.

 

Kuanza kwa mwaka hakubadili­shi mipango bali kunakufanya uzidi kutafuta njia mpya za kukamilisha mi­pango ambayo ulikuwa umeanza kui­fanya wakati mwaka unaanza.

Hivyo katika kila jambo ambalo uli­panga kulifanya mwaka ambao ume­katika, basi una nafasi ya kujipanga na kuanza upya tena kwa kasi ya ajabu ili mwaka huu nao ukiisha uwe umefikia malengo yako.

 

Nikizungumzia ishu za soka, kuna mambo mengi ambayo yatafanyika mwaka huu ikiwa ni pamoja na kuwa wenyeji wa mashindano ya Afcon kwa vijana ambapo timu yetu ya ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys itakuwa na jukumu la kulibakisha taji nyumbani.

 

Naamini hilo litakuwa ni jambo kubwa kwetu kwa mwaka huu hasa kwenye sekta ya michezo maana kuna nchi nane ambazo zinashiriki mashindano haya ambayo yana hadhi kubwa.

 

Kwa mwaka huu, Shirikisho la soka Tanzania (TFF) linapaswa lijipange upya kufanikisha tunafikia malengo ambayo yamepangwa.

 

Kikubwa kwa timu yetu hiyo ya vi­jana, mwaka huu ni kujipanga upya na kufanya makubwa zaidi ya mwaka uli­opita ili kudhihirisha ubora wenu.

 

Kila kitu kinawezekana kwenye ul­imwengu wa soka endapo vijana watapata muda mzuri wa kujipanga na kufanya kazi kwa juhudi wakiwa uwanjani bila kujali aina ya wapinzani ambao watakutana nao.

 

Kwa kufanya hivyo kutaifanya Tan­zania kuendelea kuwa kwenye ubora wake hasa kwenye michezo kwa kuwa itasaidia kupanua wigo wa wachezaji ambao watapata nafasi ya kucheza nje ya nchi.

Wachezaji wakijituma maana yake wanajiweka sokoni na wakifanikiwa kuingia sokoni na kutoka nje ya nchi kutafanya tuwe na wigo mpana wa wachezaji wanaocheza kimataifa.

 

Jambo lingine ambalo pia linapaswa lichukuliwe kwa uzito mkubwa ni pamoja na timu yetu ya Taifa ya Tan­zania, Taifa Stars ambayo imebakiwa na mechi moja ya kufuzu Afcon.

 

Stars inabidi ielewe kwamba he­sabu za kwenye soka bado zinawa­beba, hivyo wanapaswa watambue mwaka huu wana kazi kubwa ya ku­fanya ili kuwafunga Uganda na kuona uwezekano wa kufuzu Afcon.

Kwa kufanikiwa kushinda itakuwa ni zawadi bora kwa Watazania ndani ya mwaka huu hali itakayosaidia kuonge­za furaha kwa mashabiki wake.

 

Kazi kubwa nyingine kwa mwaka huu ni kwa timu ya Simba ambayo in­aliwakilisha Taifa la Tanzania kwenye Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mab­ingwa Afrika.

Kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, ni Simba pekee ndiyo wamesalia kwenye michuano hiyo, hivyo mna kazi kubwa ya kufanya kwa lengo la kuyawakilisha mataifa yaliyopo ukanda huu.

 

Kundi D ambalo mpo, naweza kuse­ma ni la kawaida na ni gumu, iwapo mtakwenda mkiwa mmeridhika kuto­kana na kufika hatua hiyo, matokeo yake mtaishia njiani kwa aibu.

Hesabu kali na juhudi zitawasaidia kufanya makubwa zaidi ya mlipofikia, wachezaji kazi ipo na nafasi mnayo na kila kitu mnapata ndani ya timu, hivyo kama kushindwa ni nyinyi wenyewe.

 

Simba wekeni mikakati kabambe ambayo itawafanya mvunje rekodi ya mwaka 2003 ambayo kwa mara ya mwisho ndiyo mlifuzu hatua hiyo, la­kini mkamaliza mkiwa nafasi ya tatu kwenye kundi.

Mbali na kuikumbusha Simba, pia Yanga nayo ina kazi kubwa ya kufanya kwenye ligi ili kuilinda rekodi yake.

 

Ni mara chache sana timu kuweza kulinda rekodi zake hasa kutokana na ushindani unaokuwepo.

Wachezaji msikubali kuvunjwa moyo ama kukatishwa tamaa mape­ma, muda wenu wa kufanikiwa ni sasa, tofauti zenu za mwaka jana ziwe kando, kazi iendelee bila kuchoka.

 

Hivi sasa mzunguko wa pili unaele­kea kuanza, hivyo shikilieni rekodi yenu ambayo mmeanza nayo ili mmalize msimu mkiwa vizuri zaidi.

Mwisho nimalizie na ishu ya ud­hamini mkuu kwenye Ligi Kuu Bara.

 

Kuna jambo la kutazama kwa hara­ka mwaka huu ili kupatikana kwa md­hamini huyo.

Muda unazidi kuyoyoma na hakuna jipya juu ya suala hilo huku timu zik­iendelea kuteseka.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mkumbuke ile ahadi yenu ambayo niliwasikia mkiizungumza kwamba mmepata mdhamini kutoka nje ya nchi, basi itimie haraka.

Watu wanataka kuona ligi yenye up­inzani, lakini ikitokea timu fulani ina njaa na nyingine ipo vizuri, hapo ush­indani haupo kabisa.

 

Nikutakie kila la heri wewe msomaji wangu ndani ya mwaka huu ambao naamini utakuwa wenye mafanikio makubwa kwako.

 

Kumbuka kabla ya kuweka malengo mapya, angalia yale ya mwaka jana yameishia wapi, ukiona hayajatimia, yatimize kwanza, kisha anza kutimiza ya mwaka huu.

Naamini una nguvu na uwezo pia wa kufikia mafanikio hayo. Hakuna kitakachoshindikana kwa mwaka huu kama ukiweka mikakati yako sawa.

Comments are closed.