The House of Favourite Newspapers

Dakika 810 Kagere kushangaza

 

Simba imebakiwa na mechi tisa za Ligi Kuu Bara mshambuliaji wa , Meddie Kagere, ana dakika 810 pekee za kuvunja rekodi za mabao Bongo. Dakika 810, sawa na mechi tisa, zinaweza kumfanya Kagere kuvunja rekodi ya mabao ya Amissi Tambwe wa Yanga ya msimu wa 2015/16 alipofunga mabao 21.

 

Kagere ana mabao 17, Heritier Makambo wa Yanga na Salim Aiyee wa Mwadui wanafuata na mabao 16.

 

Kama akifunga mabao zaidi ya matano, atakuwa ameivunja rekodi ya Tambwe, kazi itabaki kuvunja rekodi ya mabao 26 iliyodumu kwa miaka 20 ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.

 

Kagere anahitaji bao moja pekee kufikisha mabao 18 yaliyowahi kufungwa na Boniface Ambani wa Yanga msimu wa 2008/2009, Mussa Hassan Mgosi (Simba) msimu wa 2009/2010 na Mrisho Ngassa (Yanga) msimu wa 2010/2011.

 

Mshambuliaji huyo wa Simba anatakiwa kufunga mabao mawili kufikia rekodi za washambuliaji watatu waliofunga mabao 19, katika misimu tofauti ambao ni mshambuliaji wa Simba, Msomalia Isse Abushir msimu wa 2004/05, John Bocco (Azam) msimu wa 2011/12 na Amissi Tambwe (Simba) msimu wa 2013/14.

 

Rekodi zingine anazotakiwa kuvunja ni ile ya mabao 20 ya mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma aliyefunga mabao 20 msimu wa 2005/06. Huu ni msimu wa kwanza wa Kagere katika Ligi Kuu Bara baada ya kujiunga na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya

Comments are closed.