The House of Favourite Newspapers

Matola Aitoa Nishai Yanga, Aipiga 2-0 Moshi

YANGA jana ilichezea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa vijana wa Kocha Selemani Matola, polisi Tanzania ukiwa ni mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi.

 

Polisi Tanzania ambayo imepanda kucheza ligi kuu msimu jao, ilionyesha kupania mchezo huo mapema tu kutokana kucheza soka la kasi na la kuvutia huku wakilishambulia lango Yanga muda mwingi.

 

Yanga ilianza mechi ikiwa na wachezaji wengi wa kikosi cha pili katika mchezo huo ambao ni sehemu ya maandalizi kabla ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Polisi iliyoanza kwa kasi mechi hiyo ilijipatia bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na mshambuliaji Marcel Kaheza katika dakika ya sita kufuatia beki wa Yanga, Mustafa Seleman kuushika mpira akiwa ndani ya 18. Bao hilo lilidumu hadi wanakwenda mapumziko.

 

Kipindi cha pili, Polisi waliendelea kuonyesha kandanda safi hali iliyosababisha Yanga kufanya mabadiliko kadhaa kwa wachezaji wake. Hata hivyo licha ya Yanga kufanya mabadiliko hayo, bado Polisi waliendelea kulisakama lango la Yanga na kufanikiwa kuandika bao la pili kupitia kwa Ditram Nchimbi dakika ya 74.

 

Baada ya mchezo huo, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema: “Kikosi kilichocheza leo (jana) siyo kitakachocheza ligi, nimetumia wachezaji wapya wa kikosi cha pili ambacho ni mbadala na hata kwenye mechi yetu na Rollers hawatocheza hawa.

 

“Kwenye mechi yetu ya Jumapili (kesho) na FC Leopards ya Kenya nitafanya hivi kama nilivyofanya leo (jana) kwa kuchezesha wachezaji tofautitofauti.”

 

Kikosi kilichoanza jana cha Yanga: Ramadhan Kabwili, Mustafa Seleman, Gustava Saimon, Ally Ally, Kelvin Yondani, Abdulaziz Makame, Maybin Kalengo, Feisal Salum, David Molinga na Deus Kaseke.

Comments are closed.