The House of Favourite Newspapers

Liverpool Yaifunga Mdomo Arsenal, Yawapiga 3-1

LIVERPOOL jana iliwafunga mdomo Arsenal baada ya kuwaliza mabao 3-1 kwenye mechi ya Ligi Kuu England iliyopigwa kwenye Uwanja wa Anfield.

 

Kwa kipigo hicho, Arsenal imesimamishwa kasi waliokuwa wameanza nayo kwenye ligi ya kushinda mechi mbili mfululizo kiasi cha kufikiria kuwa pengine huu utakuwa msimu wao wa kufanya vyema.

Liverpool kwa upande wao wamedumisha ubabe wao kwa kushinda mechi ya tatu mfululizo na kubakia timu pekee ambayo haijadondosha pointi kwenye ligi.

 

Pia Liverpool imeendeleza ubabe dhidi ya Arsenal kwani ni mechi ya nne mfululizo wanawaliza kwenye Uwanja wa Anfield, ambapo sasa wamefikisha idadi ya mabao 15-2.

Liverpool iliyotwaa ubingwa wa England mara ya mwisho msimu wa 1989/90, sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi tisa wakati Arsenal imebakia na pointi zake sita. Katika mchezo wa jana, beki wa Arsenal, Luiz alichangia kuizamisha timu yake baada ya kufungisha mabao mawili na kutoa mwanya kwa straika wa Liverpool, Mohamed Salah kupachika mabao hayo.

Liverpool ilistahili kushinda mchezo huo kutokana na jinsi ilivyoweza kuidhibiti Arsenal na pia kuwasha mbulia vikali. Beki wa Liverpool, Joel Matip ndio alianzisha mvua ya mabao katika dakika ya 41 baada ya
kufunga kwa kichwa alipounganisha kona ya Trent AlexanderArnold  Mohamed Salah alifunga bao la pili kwa penalti katika dakika ya 49, ambapo ilitolewa baada ya kuvutwa jezi na Luiz wakati akielekea kufunga.

 

Luiz aliiponza Arsenal tena kulizwa bao la tatu baada ya kulambwa chenga na Salah, ambaye alichanja mbuga na kufunga kiulaini katika dakika ya 59. Lucas Torreira aliipatia Arsenal bao la kufutia machozi mnamo dakika ya 85 baada ya kupiga shuti lililotinga wavuni baada ya kupokea pasi ya PierreEmerick Aubameyang

Comments are closed.