The House of Favourite Newspapers

Miraji: Silaha Ya Aussems, Mbeba Mikoba Ya Okwi

Straika Miraji Athuman ‘Shevchenko’ au Sheva.

MACHUNGU ya kidonda cha mashabiki wengi wa Simba cha kumpoteza straika wao kipenzi, Emmanuel Okwi raia wa Uganda yanaanza kupoa kutokana na uwepo wa straika Miraji Athuman ‘Shevchenko’ au Sheva.

 

Awali, kabla ya Miraji, wengi walijua kwamba straika Mcongo Deo Kanda ndiye angechukua mikoba ya Okwi aliyetimkia Al Ittihad ya Misri lakini imekuwa kinyume chake na sasa wanamtazama Miraji kama mtu wao muhimu katika kuwapatia matokeo mazuri.

 

Miraji ambaye alikuwa kwenye kikosi cha dhahabu cha vijana cha Simba kilichotwaa ubingwa wa ABC Super8 Cup 2012, alionyesha kwamba anafaa kuchukua mikoba hiyo baada ya kuisaidia Simba kupata sare ya bao 1-1 kwenye mechi na UD do Songo ya Ligi ya Mabingwa lakini wakatolewa kwa sheria ya bao la ugenini.

Championi Jumatatu, linakuchambulia matukio ya Miraji ambayo ameyafanya kiasi cha kuwakuna mashabiki wa timu hiyo na kumuona mkombozi wao mpya.

 

ASABABISHA PENALTI NA DO SONGO

Kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Simba walikuwa na wakati mgumu kutokana na hadi dakika ya 86 kutofunga bao lolote kabla ya Miraji kuja kusababisha bao lao.

Miraji ambaye msimu uliopita alikuwa Lipuli FC ya Iringa, aliingia dakika ya 62 kwenye mechi hiyo akichukua nafasi ya Sharaf Shiboub kisha dakika ya 86 akaenda kusababisha penalti pekee ambayo ilizalisha bao la Simba lililofungwa na Erasto Nyoni.

 

AWAUA JKT TANZANIA

Miraji kuonyesha kwamba yuko moto kwenye mechi yake ya kwanza ya ligi akiwa na Simba aliwachapa JKT Tanzania kwenye mechi iliyoisha kwa mabao 3-0. Mabao mengine yalifungwa na Meddie Kagere.

Kwenye mchezo huo Miraji ambaye anatumia jezi namba 21 akiwa kikosini hapo alitokea benchi kisha baadaye alifunga bao ambalo liliwapa uhakika Simba wa kupata pointi zake tatu kwenye mechi ya kwanza ya ligi.

 

AWALAZA NA VIATU MTIBWA

Ijumaa iliyopita wakati Mtibwa Sugar wakijua tayari wamewaweza Simba na wataenda nao sare ya bao 1-1, mambo yalibadilika baada ya kulizwa na Miraji ambaye alifunga bao la pili la Simba kwenye mechi hiyo na kuipa timu yake ushindi wa mabao 2-1.

 

Mshambuliaji huyo alikuja kugonga msumari wa pili na wa mwisho kwa Simba kwenye mechi hiyo na kuifanya klabu yake kukusanya pointi sita ikiwa moja ya timu ambazo ziko juu kwenye msimamo.

 

MZEE WA MABAO YA MWISHO

Kutokana na mwenendo wake Miraji tayari ameshapachikwa jina la Mzee wa Mabao ya Mwisho, kwani ndiye mchezaji ambaye anafunga au kusababisha mabao ya mwisho kwenye mechi zao kila mara.

Alianza na kusababisha bao dakika ya 86 dhidi ya Do Songo, kisha dhidi ya JKT Tanzania akafunga bao la tatu na hata kwenye mechi na Mtibwa ndiye aliyefunga bao la pili na la mwisho kwa timu yake.

SILAHA YA AUSSEMS

Kocha wa Simba, Patrick Aussems amekuwa akimtumia Miraji kama silaha yake pale anapoona mambo yamekuwa magumu. Alimtumia kama silaha kwenye mechi na Do Songo, JKT na Mtibwa ambapo kwenye mechi zote alifanya kile ambacho kocha huyo alitaka kwa kufunga mabao na kuipa timu yake pointi.

 

MTOTO WA NYUMBANI

Kitu ambacho unaweza ukawa hujui ni kwamba Miraji ni mtoto wa nyumbani pale Simba. Alianza soka lake Simba ya watoto (Simba B) na alikuwa kwenye kile kizazi cha dhahabu cha Simba kilichochukua ubingwa 2012.

Kikosi hicho kiliwajumuisha Jonas Mkude, Said Ndemla, Miraji Athuman, Haroun Chanongo, Edward Christopher, Omary Salim, Miraj Adam, Abdallah Seseme, Hassan Isihaka na wengineo.

 

MWENYEWE ANAFUNGUKA

“Mimi kwenye mechi wakati nikiwa benchi huwa na kawaida ya kuwasoma wapinzani juu ya makosa ambayo wanayafanya na ndiyo imekuwa silaha yangu kubwa ninapoingia ninafanya vizuri na kufunga.

 

“Lakini pia mara nyingi kocha Aussems amekuwa akinipa maelekezo ya kwamba ninatakiwa kuomba mipira na kushambulia kwa kwenda mbele ndiyo maana ninafunga kwenye mechi zetu,” anasema Miraji.

 

MATOLA AMFUNGUKIA

Kocha wa zamani wa Miraji akiwa Simba B, Selemani Matola ambaye ni mchambuzi wa gazeti hili la Championi, amefunguka juu ya kiwango cha straika huyo kama ifuatavyo: “Ninampongeza sana kwa kiwango anachokionyesha kwani ni tangu alipokuwa timu B. Hashuki kiwango chake kwa muda wote ambao nimemjua lakini ninaona kabisa akiwa msaada mkubwa kwa Simba.

 

“Wakati akiwa Simba B ndiyo alikuwa staa wangu na anajiamini, atakuwa msaada mkubwa, ninamuona akifanya vizuri hapo na atakuwa bora zaidi ya wachezaji wengi ambao amewakuta hapo.”

STORI NA SAID ALLY, CHAMPIONI JUMATATU

Comments are closed.