Wakazi wa Kyela Ndani na Nje ya Nchi (Kyela IBHASA) Watoa Msaada wa Taulo za Kike

Baadhi ya wanafunzi wa kike katika shule 109 za msingi na sekondari, Halmshauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, wanalazimika kukatisha masomo kila mwezi wanapokuwa kwenye kipindi cha hedhi kutokana na ukosefu wa taulo za kike, hali inayowaathiri kimasomo na kisaikolojia.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Umoja wa Wakazi wa Kyela wanaoishi ndani na nje ya nchi (Kyela IBHASA) umetoa msaada wa taulo za kike zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tatu kwa wanafunzi hao, ili kuwawezesha kusoma kwa utulivu na kuhudhuria masomo kikamilifu.
Akikabidhi msaada huo, Desemba28, 2025, Mwenyekiti wa IBHASA, Lusako Mwanjejele, amesema taulo hizo zimenunuliwa kwa michango ya wanachama wa umoja huo, ambao kila mwaka hukutana Kyela kusaidia jamii.

“Msaada huu ni sehemu ya jitihada zetu za kuhakikisha watoto wa kike wanapata mazingira rafiki ya kujifunzia. Sambamba na hilo, tumekabidhi pia vifaa tiba kwa Halmashauri kwa ajili ya kusaidia maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya,” amesema Mwanjejele.
Ameeleza kuwa ni mwaka wa miaka saba mfululizo, Kyela IBHASA imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo utoaji wa taulo za kike, utunzaji wa mazingira kwa kugawa miche ya aina mbalimbali, utaoji madawati pamoja na bima za afya kwa familia zinazotoka mazingira magumu.
Akipokea msaada huo Desemba 28, 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Kenneth Mzirano, amesema ukosefu wa taulo za kike ni miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha mahudhurio hafifu shuleni kwa wanafunzi wa kike.
Ameongeza kuwa msaada huo unaunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya elimu na kulinda haki ya mtoto wa kike kupata elimu bila vikwazo.

