×

Mkude Awazimia Simu Simba SC

mkudeMwandishi Wetu, Dar es Salaam

HAKIKA unaweza kushangazwa na namna Simba inavyohaha kuwa­bakiza vijana iliowalea na taarifa zinasema kijana aliyepewa unahod­ha, Jonas Mkude amewazimia simu viongozi wa klabu hiyo.

Habari za uhakika zinasema, Sim­ba wamekuwa wakihaha kumpata Mkude ili kumalizana naye katika suala la usajili, lakini yeye alikuwa amezima simu tangu Jumatatu.

“Kweli Mkude alizima simu kabisa baada ya kuwa tumefanya naye ma­jadiliano kwa mara ya kwanza. Ku­kawa hakuna mwafaka sahihi, wakati tunasubiri arudi kumalizana naye, akazima simu.

“Tulimtafuta kwa siku mbili, mwisho tu­kawaambia Meneja Mussa Mgosi na Mrat­ibu, Abbas Ally kumtafuta. Nao wakafanya hivyo bila ya mafanikio na mwisho tumea­mua kukaa kimya na kusubiri,” chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba kilieleza.

“Sasa kama anataka kusaini sawa, au tumesikia kuna mtu kamshawishi asisaini ili akacheze Afrika Kusini sawa. Tunajua namna ya kulifanyia kazi hili na kupata jibu. Tumechoka kufanywa kama watoto.”

Imeelezwa, ili kuongeza mkataba Mkude alikuwa akitaka kupewa Sh milioni 80, baadaye akashuka hadi 60 wakati Simba walikuwa wameishia 40, wakapanda hadi 50 na Mkude ndiyo akaamua kuzima simu.

Wiki hii mwanzoni, Mkude aliliambia gazeti hili atakwenda kusaini Yanga badala ya Simba kama hali ya kutofi­kia mwafaka itaendelea.

Lakini siku chache baadaye, Maka­mu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga naye akatoa kauli yake kwamba hawana mpango na Mkude na wa­naangalia mbali zaidi kwa kusaka vi­ungo ‘wakata umeme’ wenye uzoefu kwa ajili ya michuano ya kimataifa na inaelezwa hiyo inaweza ikawa saba­bu ya kumtia hofu Mkude na huenda akaanza kuwatafuta viongozi wa Sim­ba, ili wamalizane.

Inaripotiwa kuwa juzi na jana Mkude alikuwa mmoja wa wachezaji wa Simba walioshiriki katika mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi jijini Dar.